Kazi ya ukarabati mkubwa wa sehemu zilizoathirika zaidi katika barabara ya Lusahunga –Rusumo Km 95.4 ikiendelea mkoani Kagera.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Nyakanazi-Ushirombo Km 110 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhe. Elius John Kwandikwa akiteta jambo na mkandarasi wa Nyanza Roads Works anayejenga kwa kiwango cha lami barabara ya Nyakanazi-Kibondo Km 50 ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Kidahwe-Kasulu-Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 296.
Muonekano wa nguzo za msingi wa daraja la Muyovosi linalounganisha mikoa ya Kagera na Kigoma kupitia wilaya za Biharamulo na Kakonko ambalo ujenzi wake unaendelea katika barabara ya Nyakanazi-Kibondo Km 50.
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma (wapili kushoto) akisisitiza jambo kwa mkandarasi Nyanza Roads Works anayejenga daraja la Muyovosi katika barabara ya Nyakanazi-Kibondo Km 50 (wapili kulia), ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhe. Elius John Kwandikwa akifuatilia.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Nyakanazi-Kibondo Km 50 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea barabara hiyo inaunganisha mikoa ya Kagera na Kigoma kupitia wilaya za Biharamulo na Kakonko.
Kazi ya ujenzi wa barabara ya Nyakanazi-Kibondo Km 50 ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya Kidahwe-Kasulu-Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 296 ikiendelea.
…………………….
SERIKALI imemtaka mkandarasi Nyanza Road Works anayejenga barabara ya Nyakanazi-Kibondo km 50, kukamilisha barabara hiyo ifikapo Januari mwakani.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhe. Elius John Kwandikwa amesema hayo mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo ambapo amesisitiza hakuna muda utakaoongezwa kwa mkandarasi huyo kwa sehemu hiyo ya barabara.
“Fedha unazodai tumekulipa hivyo hakikisha unatukabidhi barabara hii mapema januari 2020 kama mkataba unavyoonesha”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Aidha amewataka mameneja wa Wakala wa Barabara TANROADS wa mikoa ya Kagera na Kigoma kumpa ushirikiano wakutosha ili kukamilika kwa barabara hiyo kuwe sambamba na kukamilika kwa daraja la Muyovosi ambalo ni sehemu ya ujenzi wa barabara kabla ya msimu wa mvua nyingi.
Barabara ya Nyakanazi-Kibondo Km 50, ni sehemu ya barabara kuu ya Kidahwe-Kasulu-Kibondo-Nyakanazi yenye urefu wa KM 296 ambayo ni barabara ya kimkakati na kiuchumi kwa mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita na Shinyanga.
Naye Meneja wa TANROADS mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma amemhakikishia Naibu Waziri Kwandikwa kuwa mkoa wake umejipanga kikamilifu kusimamia miradi yote ya barabara ili kuufungua kiuchumi kwa kuhuisha huduma za kilimo, uvuvi, utalii, biashara na uchukuzi.
Naibu Waziri Kwandikwa yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Kigoma katika kukagua na kutoa maelekezo kwenye miradi ya miundombinu mkoani humo.