Home Siasa WAZIRI JAFO ATOA TAHADHARI MAPEMA KUHUSU UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

WAZIRI JAFO ATOA TAHADHARI MAPEMA KUHUSU UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

0

Na Alex Sonna, Dodoma.

Wakati tunaelekea katika uchaguzi wa serikali za Mitaa mwishoni mwa mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI) Selemani Jafo, amewatahadharisha Wakurugenzi wa halmashauri zote nchi kwenda kusimamia na kuzingatia matumizi sahihi ya fedha zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya uchaguzi huo.

Aidha amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa kote nchini kuwa makini na wasikubali kuharibiwa na watendaji wao wa ngazi za chini, na kutaka wakaratibu vizuri uchaguzi huo katika maeneo yao.

Waziri Jafo ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili kwa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa halmashauri zote hapa nchini waliokutana kukumbushana majukumu kwa pamoja na kujadili changamoto katika maeneo yao ya kazi ili kufanikisha zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa.

Waziri Jafo amesema ni lazima kila Mkurugenzi ahakikishe anasimamia fedha za uchaguzi na fedha hizo zitumike kwa maswala ya uchaguzi tu na si vinginevyo na kuonya kwa mtu yeyote atakayethubutu kutumia fedha hizo kwa matumizi mengine au kuzifuja.

“Lazima katika matumizi ya fedha za uchaguzi ni za uchaguzi tu na si vinginevyo, na mtu yeyote asijidanganye akatumia fedha hizo kinyume fedha hizo ni za moto kwelikweli hatutarajii matumizi nje ya uchaguzi” amesema Waziri Jafo.

Amewataka Makatibu wakuu wa mikoa yote kuhakikisha wanasimamia uchaguzi huo kikamilifu na kufuatilia na wasikubali kuharibiwa na watendaji wao na kuhakikisha wakaratibu vyema uchaguzi huo.

Amewaonya Wakurugenzi wa halmashauri watakao diliki kukwamisha uchaguzi huo na kuingilia majukumu ya wasimamizi wa uchaguzi huo na kuharibu uchaguzi huo watachukuliwa hatua za kisheria, na kuwasisitiza kuhakikisha demokrasia unachukua nafasi katika uchaguzi huo.

Amesema serikali inatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 82, ili kufanikisha uchaguzi huo, amebainisha kuwa serikali imetenga fedha hizo ili uchaguzi huo kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

Amewataka kwenda kutoa elimu ya kutosha kwa Jamii kuhusu uchaguzi huo ili watu wengi wajiandikishe katika uchaguzi huo, kwani katika uchaguzi uliopita watu walijiandikisha wachache na wanataka uchaguzi wa mwaka huu uwe wa mfano.

Aidha amewataka wazingatie ratiba zilizowekwa kuhusu  ukomo wa viongozi waliopo madarakani, kuzingatia mda wa kuanza kuandikisha kwenye daftari ya wapiga kura, tarehe ya kuchukua fomu, mda wa kukata rufaa na kusikiliza rufaa lazima ziainishwe mapema, na kuhakikisha wanasimamia demokrasia.

Amewapongeza Katibu Tawala wa Mikoa  kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuteua na kuapisha wasimamizi wa uchaguzi huo katika halmashauri zote na kubainisha kuwa alifuatilia na kuona hakukuwa na dosari, tarehe 12 waliapishwa wasimamizi na 13 mwezi wa tisa walipaswa kutangaza vituo vya uchaguzi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema mambo yote muhimu kwa ajili ya uchaguzi huo yamekamilika, ikiwamo nyenzo zitakazotumika katika uchaguzi huo, na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya uchaguzi huo.

Pia amesema licha ya serikali kuu kutenga fedha kwa ajili ya uchaguzi huo, lakini lazima kila halmashauri nayo itenge fedha kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi huo.