Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo akisalimiana na viongozi wa vijiji vya Mombose na Bubutole kata ya Farkwa Wilaya ya Chemba kabla ya kuzungumza nao kuhusu Wizara kupokea fedha shilingi bilioni 7.8 za kuwalipa fidia wananchi ili kupisha ujenzi wa bwawa la Farkwa.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo akiteta jambo na Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chemba Bwana Mohamedi Maingu kabla ya kuanza kuzungumza na viongozi.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo akizungumza na viongozi wa vijiji vya Mombose na Bubutole kata ya Farkwa Wilaya ya Chemba (hawapo pichani).
Viongozi wa vijiji vya Mombose na Bubutole kata ya Farkwa Wilaya ya Chemba wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo (hayupo pichani).
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Prof. Kitila Mkumbo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa vijiji vya Mombose na Bubutole kata ya Farkwa Wilaya ya Chemba pamoja na viongozi kutoka Wizara ya Maji na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi David Palangyo.
………………………
Serikali itawalipa fidia wananchi wa Farkwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma kiasi cha shilingi bilioni 7.8 kuanzia mwezi Oktoba, 2019 ili kupisha ujenzi wa mradi wa bwawa la Farkwa.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Prof. Kitila Mkumbo amesema hayo katika kikao na viongozi wa vijiji vya Mambose na Bubutole ambavyo wananchi wake watahama baada ya kulipwa fidia.
Prof. Mkumbo amesema serikali kupitia Wizara ya Maji hivi sasa ipo tayari kuwalipa wananchi wapatao 2,868 ambao wamefanyiwa tathmini kuanzia tarehe 16 Oktoba, 2019 ili nafasi ya kuanza utekeleaji wa Bwawa la Farkwa ipatikane.
Katibu Mkuu Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa wananchi watakaolipwa fedha hizo ambazo Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amezitenga na kuelekeza wilayani Chemba ni jambo la msingi wakihamisha shughuli zao mapema kadri watakavyofidiwa.
Wakati huo huo, Bw. Jumanne Hamisi akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kitongoji cha Kichangani kata ya Farkwa amesema wamepokea kwa furaha taarifa za Wizara ya Maji kuja kuwalipa fidia kwa sababu ni jambo walilosubiri kwa muda mrefu, kwa sababu waliacha shughuli nyingi hususan za kilimo katika maeneo yao.
Mradi wa Bwawa la Farkwa upo katika vipaumbele vya miradi inayotekelezwa na serikali na utakapokamilika utaleta fursa za kiuchumi na utaongeza upatikanaji wa maji katika Jiji la Dodoma ambalo hivi sasa linaongezeko la wakazi.