Na Jozaka Bukuku
MAFUNZO ya Ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana wajasiriamali ambayo yamegharamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu yakiratibiwa na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yamepokelewa vema na vijana wa Mkoa wa Mbeya.
Hadi wakati huu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu imeshawafikia vijana kwenye Mikoa ya Dodoma, Geita, Mwanza,Ruvuma, Songea na hivi sasa mafunzo yanaendelea kufanyika katika Mkoa wa Mbeya.
Mafunzo haya kwa mara ya kwanza yalizinduliwa rasmi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) tarehe 29 Julai 2019 katika ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma na yanatarajiwa kufikia vijana wasiopungua 1200 katika Mikoa nane ya Tanzania Bara kwa awamu ya kwanza.
Lengo la mafunzo haya ambayo yanawagusa vijana wenye rika la kuanzia miaka 18 hadi 35 ni kuwafundisha vijana wajasiriamali kujitambua kama wajasiriamali, usimamizi wa fedha, uandaaji wa andiko la mradi kwa ajili ya kupata uwezeshaji wa mitaji, namna ya kutathmini masoko na mahitaji ya mteja, kuanzisha makampuni, kurasimisha biashara ili kupanua wigo wa ajira na kuongeza tija, kuwaunganisha na fursa za uwezeshaji kupitia mifuko ya uwezeshaji ya umma na taasisi za fedha za umma na binafsi.
Miongoni mwa wadau wanaoshirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na wenye Ulemavu na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) katika kutoa mafunzo hayo ni pamoja na SIDO, OSHA,Pass Trust, Mfuko wa Misitu (TFS), Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF), Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Self Microfinance, NMB, CRDB na NBC.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mkoani Mbeya Mchumi Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Silas Daudi alisema kuwa mafunzo haya ni sehemu ya Program ya Kitaifa ya Ukuzaji Ujuzi ambayo inatekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu sehemu ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wadau.
Bwana Silas alizitaja baadhi ya program zinazotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu sehemu ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu ambazo ni sehemu ya Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi ni pamoja na mafunzo ya uanagenzi,Mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu, kutambua ujuzi uliopatikana nje ya mfumo wa elimu na mafunzo ya kuongeza ujuzi kulingana na mahitaji ya vijana.
Kupitia program hizi Ofisi ya Waziri Mkuu sehemu ya Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu imepanga kujenga kitalu nyumba (green house) kimoja kwa halmashauri zote nchini na kuwafundisha vijana 100 kila halmashauri kutumia kitalu nyumba ambavyo vitatumika kama shamba darasa kwa ajili ya vijana kujifunza teknolojia hii.
Hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu imejenga kitalu nyumba kimoja na kuwafundisha vijana 100 kwa kila halmashauri katika mikoa 12 Tanzania Bara na zoezi hili linaendelea katika mikoa 14 iliyobaki.
Aidha, Bwana Silas alieleza kuwa kundi la vijana ndiyo sehemu kubwa ya nguvukazi ya Taifa ambapo kwa mujibu wa utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014, vijana wanafanya asilimia 56 ya nguvu kazi ya Taifa.
Kwa kuzingatia umuhimu wa kundi la vijana katika Taifa, program zote zimeandaliwa maalumu kwa ajili ya kundi hili kuwawezesha kujiajiri kwa tija na kuongeza wigo wa ajira kwa vijana wengine.
“Tunaamini kupitia mafunzo haya ya ujasirimali na usimamizi wa biashara utakuwa mwanzo wa vijana kuanzisha makampuni yao ya biashara, kusimamia na kufanya biashara kwa tija na kutengenza ajira kwa vijana wengine lakini pia elimu hii itawasaidia kujua ni sifa zipi wanapaswa kuwa nazo pindi wanapozisogelea fursa za mikopo na ruzuku kutoka kwenye mifuko ya uwezeshaji”alisema Mchumi Mkuu.
Nae mjasiriamali Rosemary Kihele ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo alisema kuwa moja kati ya faida kubwa alizozipata kupitia program hii kutoka ofisi ya waziri mkuu ni kufahamu namna ya kuziendea fursa za mikopo kutoka kwenye mifuko ya uwezeshaji Serikalini.
“Hapo kabla nilikuwa sifahamu sifa zipi nastahili kuwa nazo ili niweze kupata mkopo kutoka kwenye mifuko ya uwezeshaji ili kukuza biashara yangu lakini sasa nimepata mwanga mkubwa kutokana na mafunzo haya”alisema mjasiriamali huyo.
Wakati wa uzinduzi wa mafunzo Mheshimiwa Jenista Mhagama alisisitiza vijana kuzingatia kile kinachofundishwa ili kiweze kubadili uelekeo wa biashara zao na kuwa na mchango chanya kwenye pato la Taifa.
“Serikali ya awamu ya tano chini ya Mheshimiwa Raisi John Pombe Magufuli imedhamiria kubadilisha maisha ya vijana na kupanua wigo wa ajira kwa kuboresha shughuli za ujasiriamali ambazo zimebuniwa na vijana wenyewe”alisema Mheshimiwa Mhagama.
Baada ya kumaliza mafunzo haya vijana wanatunukiwa vyeti vya ushiriki kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu lakini pia kutakuwa na zoezi la ufuatiliaji ili kupima matokeo.