**********************************
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bwa. Gabriel Malata, ameahidi kuchapa kazi kwa
bidii na kuyaenzi mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake katika kuhakikisha
ofisi yake inafikia malengo iliyojiwekea.
Ametoa ahadi hiyo mapema leo alipomtembelea Jaji kiongozi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi pamoja na ujumbe wake ofisini kwake
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, amekili kuwepo na changamoto nyingi hasa
katika kipindi hiki ambapo Tanzania kama nchi inazidi kupiga hatua katika Nyanja
zote katika kuhakikisha inafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Ukiangalia namna nchi yetu inavyopiga hatua katika sekta ya viwanda,
miundombinu kama reli, ununuzi wa ndege na miradi mikubwa ya umeme, kwa
macho ya kawaida hatuwezi kutazamwa vizur na baadhi ya watu,” alisema Bwa.
Malata.
Kiongozi huyo ameendelea kusisitiza kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
itaendelea kutekeleza kwa ufasaha yale yote yanayotakiwa kutekelezwa na serikali
hatua itakayosaidia ofisi hiyo kutoa huduma bora pamoja na kuwafikia watu wengi
zaidi.
Bwa. Malata ameongeza kuwa anatambua changamoto zilizopo kwa upande wa
mawakili na kuahidi kuzifanyia kazi haraka na kwakuanza ameahidi kuwajengea
uwezo kwa kuwaandalia mafunzo maalum yatayowasaidia kutekeleza majukumu
yako kwa ubora unaotakiwa.
Aidha, Naibu wakili Mkuu amemueleza Jaji Kiongozi, Mhe. Feleshi kuwa
inawezekana mawakili wa serikali wana mapungufu na kumhakikishia kuwa
atayashughulia mapungufu hayo ndani ya muda mufupi ujao ili waweze kuendana
na miongozo ya Mahakama hatua itakayo wasaidia wawe mifano bora kwa
mawakili wengine.
“Inawezekana timu yetu ina mapungufu ila naomba niseme tu ni kwa kipindi cha
mpito ninaahidi kuwa nitahakikisha tunainoa iendane na vigezo vinavyotakiwa,”
alisema Bwa. Malata.
Kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa unaotakiwa kufanyika baadaye mwaka huu,
Bwa. Malata amesema wanatambua jukumu kubwa walilonalo na kuahidi kuwa watahakikisha wanajipanga vizuri ili kuhakikisha serikali inapata haki yake kwa
mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Naye Jaji kiongozi wa Mahakama ya Tanzania amempongeza kiongozi huyo kwa
kuteuliwa kushika nafasi hiyo na kumsihi kufanya kazi kwa bidi huku akifuata
sheria na taratibu ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha na kwa weledi
zaidi kwa manufaa ya taifa.
“Malata umefanya kazi muda mrefu serikalini, una uzoefu wa kutosha kafanye
kazi kwa weledi utimize majukumu yako vizuri,” alisema Mhe. Jaji kiongozi.
Jaji Kiongozi pia ameishauri Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa na mfumo
madhubuti utakaoisaidia ofisi hiyo kufuatilia kesi hasa zile za mikoani ili waweze
kuzishughulikia kirahisi kesi zote zilizofunguliwa dhidi ya serikali katika mikoa
yote.
Vilevile Jaji Kiongozi amewaomba viongozi wa Ofisi hiyo kwa kushirikiana na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na mwendesha mashtaka wa serikali
kukaa pamoja na kufanya utafiti wa kina ili waweze kubaini sheria zote zilizopitwa
na wakati na zile zenye mapungufu ili waweze kuziwasilisha bungeni kwa lengo la
kuzifanyia maboresho.
Wakati huohuo Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Clement Mashamba amemshukuru
Mhe. Jaji Kiongozi kwa ushirikiano ambao amekuwa akiwapa huku akiahidi
kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wenzake katika kuhakikisha kuwa
wanafikia malengo mbalimbali waliyojiwekea.