Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt John Jingu akiangalia moja Sehemu za Jengo la Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo nje Kidogo ya Manispaa ya Iringa ambacho kinaendelea na ukarabati wa baadhi ya Majengo yake ili kuweka mazingira mazuri ya kujifunza kufundishia chuoni hapo.
Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Vyuo vya Maendeleo ya Jamii Bi.Neema Ndoboka kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii akizungumza na watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo nje Kidogo ya Manispaa ya Iringa hawapo pichani.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo nje Kidogo ya Manispaa ya Iringa hawapo pichani.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akipokea maelezo kutoka kwa Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa Bi. Josephine Mwaipopo kuhusu umuhimu wa mchezo wa Bembea kwa watoto na namna unavyotumika kuweka vizuri watoto kisaikolojia alipotembelea Ofisi mpya ya Maafisa Ustawi wa Jamii iliyoko halmashauri ya Mji wa Iringa.
Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
……………….
Na Mwandishi Wetu Iringa
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Mkuu Maendeleo ya Jamii Dkt.John Jingu amevitaka vyuo vya Maendeleo nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuvitaka kuzalisha wataalam watakaoweza kujiajiri lakini pia kuleta mabadiliko katika Jamii inayozungaka vyuo ili Jamii ione umuhimu wa kuwepo kwa vyuo hivyo.
Dkt.Jingu amesema hayo wakati wa ziara yake Mkoani Iringa alipotembelea chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kukutana na wafanyakazi lakini pia kujionea kazi zinazoendelea chuoni hapo.
Katika mazungumzo yake na wafanyakazi hao Dkt.Jingu amesema kuwa lazima vyuo vya Maendeleo ya Jamii viwe na tofauti na vyuo vingine kwa kuwa wataalam wake wana wajibu wa kuchechemua Maendeleo katika Jamii wanazoishi.
Pamoja na mazungumzo yake kwa wafanyakazi hao Dkt.Jingu amesema hajaridhishwa sana na namna Chuo cha Ruaha kinavyotumia fursa zilizopo kushirikisha Jamii inayowanguka hivyo kuwataka kuzidisha juhudi ili Jamii yenyewe ione chuo hicho kina umuhimu kwa Jamii.
Dkt. Jingu pia ameutaka uongozi Chuoni hapo kuhakikisha unazingatia matumizi bora ya rasilimali fedha na kufuata taratibu za manunuzi wakati wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya Chuo hicho.
“Akikisheni mnafanya kazi za ukarabati wa Majengio kwa kuzingatia thamani ya fedha kwa kuwa wataalamu wa uthamanishaji watafanya ukaguzi kuangalia kama kazi inayofanyika inaendana na thamani ya fedha”. Aliongeza Dkt. Jingu.
Awali akitoa taarifa ya Chuo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Bw.Godfrey Mafungu alisema chuo hicho kishirikiana na Kijiji cha Ikuvilo Jilani na chuo hicho kama kijiji cha mfano na kuhamasisha Jamii ya Kijiji hicho kushiriki katika kujiletea Maendeleo.
Aidha Bw. Mafungu pia katika taarifa yake alisema chuo chake kinaendelea na ukarabati wa majengo chakavu ya Chuo pamoja na kuwepo changamoto ya Rasilimali Fedha.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu anaendelea na Ziara ya Siku Tano katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kutembelea vyuo vya Maendeleo ya Jamii na pia Makazi ya Wazee yaliyoko katika Mikoa hiyo.