*****************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inahitaji watumishi waadilifu wenye uwezo wa kufanyakazi kwa uaminifu na waliotayari kuwahudumia wananchi wote bila ya ubaguzi.
Amesema Serikali inataka kuona watumishi wa umma wakitumia taaluma zao katika kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi kwenye maeneo yao hususani wa vijijini, hivyo amewataka watenge muda wa siku nne kwa ajili ya kukutana nao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 26, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga pamoja na Madiwani kwenye mkutano uliofanyika Halmashauri ya Mufindi.
Amesema watumishi hao wanapaswa kutekeleza matakwa ya ilani ya CCM, ambayo imeainisha kila kitu kinachotakiwa kufanyika katika halmashauri, hivyo wakuu wa idara hawanabudi kuisoma kwa makini ili waweze kupata mafanikio kwenye utendaji wao.
Waziri Mkuu amesema ni lazima watumishi hao wafanye kazi za Serikali na waache itikadi zao watekeleze ilani ya CCM. “Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri hakikisheni wakuu wa idara na wasaidizi wao wanawahudumia wananchi.”
“Tuelewane vizuri hapa, msimamo wa Serikali hii ni kuchapakazi mtu atakaye vurugavuruga hana nafasi katika Serikali hii na hatuta muundia tume tutamalizana naye hapo hapo. Rais wetu anataka kuona wananchi wakihudumiwa katika maeneo yao.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amezitaka halmashauri nchini zinapotoa huduma zihakikishe zinapotoa huduma kwa wananchi wasisahau kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa ajili ya makundi maalumu kama wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Pia, Waziri Mkuu amewataka watendaji hao kutofanyakazi kwa mazoea, ambapo amemtaka Mhandisi wa Maji wa Wilaya ya Mufindi kuhakikisha anasimamia vyanzo vyote vya maji na kuwachukulia hatua watu wote wanaolima au kufanya shughuli katika vyanzo vya maji. Amesema kata ya Igowole iwe imepata maji ifikapo 2020.
Katika hatua nyingine,Waziri Mkuu amesema suala la ukusanyaji wa mapato limepewa kipaumbele na Serikali kwa sababu linasaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Madiwani msimamie ukusanyaji mapato na hakuna kumlinda mtu anayetafuna fedha hizo.”
Amesema watendaji nao wahakikishe wanawasimamia vizuri mawakala waliopewa zabuni za ukusanyaji wa mapato na watakaobainika kushindwa kutekeleza vizuri jukumu hilo wasipewe tena zabuni na badala yake watafutwe wazabuni watakaokusanya vizuri.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Joseph Kandege amesema utendaji wa kazi katika hospitali ya wilaya ya Mufindi si wa kuridhisha hasa siku za Jumamosi, amewataka watumishi wabadilike kwani huduma zinatakiwa wakati wote.
Awali,Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi amesema hali ya upatikanaji wa huduma za afya katika halmashauri ya Mji wa Mafinga si ya kuridhisha kutokana na uhaba wa watumishi kwani waliopo ni 204 huku mahitaji yakiwa 310. Waziri Mkuu amesema suala hilo linafanyiwa kazi, Serikali inaendelea kuajiri.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Happi amesema halmashauri za wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga zinafanya vizuri katika sula zima la ukusanyaji wa mapato pamoja na kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya wanawake, vijana na wenyeulemavu.
Akizungumzia kuhusu hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Mafinga amesema inachangamoto ya utoaji wa huduma kwa sababu ya kuhudumia halmashauri mbili ya Mufindi na Mafinga lakini mgawo wa dawa wanaopewa ni kwa ajili ya wakazi wa Mafinga pekee.
Pia, Mkuu wa mkoa ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kupeleka zaidi ya sh. bilioni saba katika wilaya hiyo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga.
Baada ya kuzungumza na watumishi, Waziri Mkuu amekagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospiyali ya wilaya ya Mufindi inayojengwa katika Kijiji cha Nzivi kata ya Igowole. Ujenzi wa hospitali hiyo utagharimu sh. bilioni 1.5 na upo katika hatua za umaliziaji.