*************************************
Na Ales Mbilinyi – JKCI
26/9/2019 Kwa mara ya kwanza hapa nchini umefanyika upasuaji wa moyo wa kukamilisha kuunganisha mfumo wa mzunguko wa damu iliyokwisha kutumika mwilini kwa kuunganisha mishipa hiyo ya damu kwenda moja kwa moja kwenye mapafu ili ikasafishwe bila kupitia mfumo wa usukumaji wa upande wa kulia wa moyo (Fontan operation).
Upasuaji huo ambao ulichukuwa muda wa masaa sita ulifanyika kwa mafanikio makubwa umefanywa jana katika kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanywa na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikia na wenzao wa shirika la Mending’s Kids International lenye wataalamu wa afya kutoka nchini Italia na Marekani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Anjela Mhozya alisema mtoto aliyefanyiwa upasuaji huo anaumri wa miaka minne alikuwa na tatizo la kutokuwepo kwa valvu ya kulia ya tricuspid na mfumo wa moyo wa kulia ambao ulikuwa mdogo kuliko kawaida (tricuspid atresia).
“Tangu kuanza kwa kambi hii siku ya jumatatu jumla ya watoto 35 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu ya moyo kutokuwa katika mpangilio maalum wamefanyiwa upasuaji wa kufungua na bila kufungua kifua ambapo hali zao zinaendelea vizuri na wengine wamesharuhusiwa kutoka katika chumba cha wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na dawa pamoja na mazoezi”,.
“Kati ya watoto 35 waliofanyiwa upasuaji watoto 20 wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua kwa kutumia mtambo wa Cathlab na 15 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua”, alisema Dkt. Anjela ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa walioko ICU.
Dkt. Anjela alisema ujio wa madaktari hao kutoka nchini Italia na Marekani umekuwa ni neema kwao kwani kumewasaidia kuongeza ujuzi wa kazi na mara baada ya kumalizika kwa kambi hiyo watautumia ujuzi huo katika kazi zao za kila siku.
Kwa upande wake Balozi wa Italia nchini Mhe. Roberto Mengoni ambaye alitembelea Taasisi hiyo ili kuangalia maendeleo ya kambi hiyo aliipongeza JKCI kwa huduma za matibabu ya moyo inazozitoa hasa kwa watoto ambao ni taifa la kesho.
“Nafahamu kuwa Taasisi hii inategemewa na watanzania pamoja na nchi jirani na ndiyo maana katika kambi hii kuna watoto kutoka nchini Ethiopia na Malawi ambao wamekuja kutibiwa na kama nilivyowaona hali zao zinaendelea vizuri baada ya kupata matibabu”,.
“Hongereni sana kwa kazi mnayoifanya ya kuokoa maisha ya watanzania wenye matatizo ya moyo. Tanzania inafanya vizuri katika sekta ya afya nampongeza Waziri wenu Mhe. Ummy Mwalimu mara kwa mara nimekuwa nikimuona akifanya kazi mbalimbali za kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora za afya”, alisema Mhe. Mengoni.
Nao wazazi ambao watoto wao wametibiwa katika kambi hiyo waliishukuru Serikali kwa Kuboresha huduma za matibabu ya moyo hapa nchini na kuwataka wazazi wengine ambao watoto wao wanamatatizo ya moyo kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)ambako kuna wataalamu wa kutosha.
Upendo Samweli kutoka Iringa ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua alisema mtoto wake alikuwa anapata tabu ya kupumua vizuri, kukohoa mara kwa mara na kupungua uzito lakini baada ya kufika JKCI na kufanyiwa vipimo alikutwa na tundu kwenye moyo.
Upendo aliomba, “Ninawaomba madaktari walioko mikoani wanaowatibu watoto kama wataona wanamtibu mtoto kwa muda mrefu hapati naafuu wampe rufaa ili aweze kutibiwa katika Hospitali zenye utaalamu wa juu zaidi. Mimi mwanangu kabla hajagundulika kuwa na matatizo ya moyo niliambiwa mtoto hapati lishe ya kutosha, kanywa maji ya uzazi lakini baada ya kuona anatibiwa muda mrefu bila ya kupata naafuu niliomba rufaa ya kuja kutibiwa JKCI”,.
Naye Rachel Anton mkazi wa Kibaha ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji mkubwa wa kuziba tundu kwenye moyo na kurekebishwa mishipa ya damu ya moyo alishukuru kwa huduma ya matibabu aliyoipata na kuwasihi wazazi wanapoona mtoto hakui vizuri na anaumwa mara kwa mara wawahi Hospitali mapema ili aweze kutibiwa kwa wakati.