Na Silvia Mchuruza,Kagera;
Ili kuhakikisha lazima wekundu wa Msimbazi Simba wanaziacha pointi tatu kwa wenyeji Kagera Sugar,Mkuu wa Mkoa Kagera Brig. Jen. Marco E. Gaguti,ametembelea kambi ya timu hiyo na kuwapa hamasa na morali wachezaji na benchi la ufundi kuwa pointi tatu muhimu zinahitajika.
RC Gaguti akiwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Missenyi ameungana na Kagera Sugar kufanya mazoezi ya pamoja huku akiwasisitizia kuwa Serikali ya mkoa ipo nao katika kuifunga Simba Siku ya Alhamisi mechi ya Ligi Kuu Vodacom.
“Ligi ndo imeanza hivyo Maombi yangu kwenu ni kuona Msimu huu wa 2019 na 2020 hakikisheni Kombe linakuja Mkoani Kagera sababu mnayo na mnaweza”Amesema RC Gaguti
Aidha Rc Gaguti amewaelekeza wakuu wa wilaya za Missenyi na Bukoba kuipa sapoti timu ya Kagera Sugar siku ya Alhamisi ikiwa inaingia uwanjani kumenyana na Simba.
Hata hivyo RC Gaguti ametoa wito kwa wanakagera pamoja na wakazi wa kanda ya Ziwa kujitokeza kwa wingi ili kuujaza uwanja na kuishingilia kwa nguvu timu yao ili iibuke na ushindi dhidi ya Simba toka Dar es Salaam.
Kwa upande wake Nahodha Juma Nyosso amesema maandalizi yamekamilika na wapo tayari kuikabili Simba, huku akizidi kuomba mshikamano huo uendelee hata kwa mechi nyingine na hata pale Timu itakapoteleza kwani mpira wa miguu una matokeo matatu.
Kagera Sugar wameanza Ligi kwa kucheza ugenini mechi tatu na kushinda zote na Timu ya Simba inatarajia kuwasili leo mjini Bukoba tayari kwa vita huku ikiingia kwa tahadhari kwani msimu uliopita ilifungwa zote mbili.