Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Mkoani Manyara Hudson Kamoga, akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo jipya la utawala linaloendelea kujengwa katika kata ya Dongobesh kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo, katikati ni mbunge wa jimbo hilo Flatei Massay.
******************************
Na Mwandishi wetu, Mbulu
Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo amesema katika wakurugenzi wanaofanya vizuri, wanaojitahidi kutekeleza na kusimamia shughuli zao kikamilifu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara Hudson Kamoga naye ni mtendaji mzuri.
Jafo aliyazungumza hayo alipokuwa kwenye ziara yake ya kikazi katika halmashauri hiyo, ambapo aliweza kitembelea jengo jipya la utawala
linaloendelea kujengwa katika kata ya Dongobesh na kutembelea jengo la hospitali ya wilaya.
Waziri Jafo alisema kuwa ni ukweli usiopingika kuwa katika wakurugenzi wanaofanya vizuri, wanaojitahidi kusimamia na kutekeleza majukumu yao kikamilifu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga anajitahidi sana hasa ikizingatiwa ametoka katika sekta binafsi na siyo serikalini.
AmWaziri Jafo alisema Rais Dk.John Pombe Magufuli alimuamini Kamoga na kumpa dhamana katika halmashauri ngumu ya wilaya ya Mbulu, kitendo ambacho amesema amepata bahati kupewa halmashauri ngumu ambapo huko ndio amekwenda kupikwa ili aonekane kama ataiweza.
“Kwa dhati ya moyo wangu kabisa nikupongeze sana Kamoga, wakati ule na kipindi chako cha 360 ulikuwa mkosoaji sana aaah sasa wakurugenzi vipi mbona mambo hayaendi, tukasema huyu lazima tumpachike hapa, lakini nikushukuru mheshimiwa Rais John Magufuli alikuamini na wewe amekupa dhamana katika halmashauri hii ngumu , maana wewe umepata bahati, bahati yenyewe ni nini umepewa halmashauri ngumu na mpya kwako, kwa hiyo kama huku umekuja kupikwa kweli uonekane kama je kweli unaweza? alihoji Waziri Jafo.
Alisema amekwenda Mbulu kuhakikisha angekuta ujenzi wa jengo jipya la utawala halijaanza, angeondoka na fedha, lakini cha ajabu amekwenda kukagua na kukuta kazi imetekelezeka kwa asilimia 49, ameridhishwa na kazi nzuri zinazoendelea katika mradi huo pamoja na mradi wa hospitali ya wilaya.
“Katika wakurugenzi wanaofanya vizuri, wanaojitahidi kama binadamu wote tunamakosa yetu, tuna mapungufu yetu, hakuna binadamu aliye perfect Kamoga anajitahidi sana, hongera umepata muda wa kujifunza kazi na unaendelea na kazi, haya majengo haya nilikuwa naangalia hapa, umeprove kwamba wewe sasa umeshawiva katika hii kazi, na nimeridhishwa na ujenzi wa miradi hii kwa asilimia 100” alisema Waziri Jafo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Mbulu Hudson Kamoga alisema ujenzi wa jengo hilo la utawala ulianza rasmi Aprili 15, mwaka huu ambapo kwa sasa kwa hatua ya ujenzi imefikia asilimia 40 na tayari wameshatumia sh.bil. 1
Kamoga alimpongeza Waziri Jafo kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kusimamia wizara yake lakini pia alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwapelekea fedha za miradi hiyo, na hivyo wananchi wa Mbulu wameanza kuona mabadiliko makubwa katika halmashauri yao.
“Mheshimiwa Waziri nikushukuru sana wewe na nikupongeze kwa jitihada kubwa ambazo unazifanya katika kusimamia wizara, lakini pia kwa nafasi ya pekee kabisa nimshukuru sana mheshimiwa Rais Magufuli kwa kutuletea fedha hizi na wananchi wa Mbulu sasa wanaona Mbulu inabadilika.