Serikali imesema imedhamiria kuhakikisha wadau wa sekta ya uvuvi nchini wanapata fursa zilizopo katika sekta hiyo kwa kutambuliwa katika mfumo ulio rasmi ili waweze kuchukua mazao ya samaki yatakayowawezesha kuinua vipato vyao.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo wakati akishuhudia utiaji saini kati ya Benki ya Posta Tanzania (TPB) na Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA) na kuzindua rasmi Wavuvi Akaunti, katika mwalo wa Igombe uliopo Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza, ambapo amewataka wadau hao kuhakikisha wanajiunga na akaunti hiyo ili waweze kupata huduma za kifedha zitakazowawezesha zana za kisasa kwa ajili ya shughuli za uvuvi ambazo zitawafanya kupata malighafi kwa wingi.
“Ninawaomba wavuvi mfungue Wavuvi Akaunti katika Benki ya Posta Tanzania (TPB) itakuwa rahisi kwenu kupata msaada ili muweze kufanya biashara ambapo viwanda sasa vimeanza kufufuliwa upya, nasi tumeagiza kwa sasa samaki wote wanaozalishwa katika viwanda vyetu ni lazima wasafirishwe moja kwa moja kwenda nchi za nje kupitia viwanja vyetu vya ndege badala ya kusafirishwa kwenda nchi zingine kupitia viwanja vya ndege vya nchi jirani.” Amesema Mhe. Ulega
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania (TPB) Bw. Sabasaba Moshingi alisema utiaji saini kati ya benki hiyo na Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA), ni muhimu kwa kuwa huduma ya Wavuvi Akaunti itawawezsha wavuvi wengi kuwa na utaratibu wa kutumia huduma za kibenki kwa kuwa kwa sasa wengi wao utumiaji wao wa huduma za kibenki upo chini.
Naye Katibu wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wavuvi Tanzania (CHAKUWATA) Bw. Bakari Kadabi aliwaomba wananchi wote kuungana kutokomeza uvuvi haramu na kuuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kuongeza mnyororo wa thamani kwa wavuvi na vikundi kujiunga na chama kikuu ambapo mkataba huo na TPB utawawezesha wadau wa sekta ya uvuvi kupata elimu ya fedha na kukopeshwa na benki hiyo kwa ajili ya uendelezaji wa kazi zao.