Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwasikiliza Wafanyabiashara wa Madini katika Soko dogo la Madini Katoro wakati kamati hiyo ilipotembelea soko hilo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mariam Mzuzuri (kushoto) akifuatilia hoja zilizokuwa zikitolewa na Wafanyabiashara wa Soko la Madini Katoro. Katikati ni Mjumbe wa Kamati hiyo Fred Mwakajoka na kulia ni Katibu wa Kamati hiyo Felister Mgonja.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akifuatilia jambo wakati Kamati ya Bunge ikiwasikiliza wafanyabishara wa madini , kamati hiyo ilipotembelea soko la madini. Kulia ni Mjumbe wa Kamati hiyo Mariam Msabaha na Kushoto ni Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda.
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo akizungumza jambo na wafanyabiashara wa soko la Madini Katoro wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
…………………..
Wafanyabiashara wa Madini katika Soko Dogo la Madini Katoro wameiomba Serikali iwaruhusu kuwa na Wasaidizi watakaowasaidia kununua madini maeneo yenye mialo ya uchenjuaji na kuwauzia kwenye vituo vya ununuzi.
Wafanyabiashara hao wametoa ombi hilo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea soko hilo kwa lengo la kujifunza na kuangalia namna masoko ya madini yanavyoendeshwa.
Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema kuwa, Sheria na Kanuni za biashara ya madini zinaelekeza kuwa shughuli za uuzaji na ununuzi wa madini zinapaswa kufanyika kwenye vituo maalum vya manunuzi hivyo suala la kuwa na wasaidizi kwenye mialo wa kuwauzia wafanyabiashara hao linakinzana na Sheria ya Madini na Kanuni za madini kwenye masoko.
‘’ Kamati ndiyo inaishauri Serikali, ndiyo Bunge na Wawakilishi wa wananchi. Tutaendelea kutatua changamoto tunazokutana nazo kwenye masoko. Sote tunajua Masoko ni Mapya, Sheria Mpya, Kanuni Mpya, hivyo tutaendelea kutatua changamoto hizo yakiwemo masuala ya vifaa na watumishi,’’ amesema Naibu Waziri Nyongo.
Aidha, Naibu Waziri Nyongo amewataka wafanyabiashara wa madini na wachimbaji kuyatumia masoko ya madini na kueleza kuwa, kufanya biashara ya madini nje ya masoko ni kujiweka kwenye matatizo. Pia, amewasisitiza kuhusu matumizi sahihi na salama ya zebaki na kueleza kuwa, serikali itaendelea kuangalia njia mbadala za teknolojia ili kuweza kuachana na matumizi ya zebaki.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mariam Mzuzuri amewataka wafanyabiashara hao kuendelea kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu wakati Serikali na Kamati zikiangalia namna ya kuzifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa kwao.
‘’ Kwa kuwa masoko haya yanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ni vyema suala hili mtuachie kwanza sisi na serikali ili tuliangalie,’’ amesema Mzuzuri. Kufuatia hali hiyo, Mzuzuri ameitaka wizara kuendelea kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara na wachimbaji wa madini ili wajue namna ya kuyatumia masoko ya madini na kujua mwenendo mzima wa shughuli za madini na biashara ya madini inavyofanyika.
Katika hatua nyingine, kamati imeitaka Serikali kuhakikisha suala la Ulinzi kwenye masoko ya Madini halisubiri michakato bali linatakiwa kufanyiwa kazi haraka kutokana na rasilimali zilizopo katika masoko hayo.
Makamu Mwenyekiti amesema hayo kufuatia ombi la kuimarishwa kwa Ulinzi katika Soko la Katoro lililotolewa na Wafanyabiashara wa Madini sokoni hapo wakati wa ziara yake mkoani Geita.
Naye, Mjumbe wa Kamati hiyo Fred Mwakajoka ametaka taasisi zote za serikali zinazoshirikiana na Tume ya Madini kuendesha masoko hayo ziwepo katika masoko hayo ili kurahisisha utendaji wa majukumu ya masoko .
Baada ya kutembelea soko la Katoro, Kamati hiyo pia imetembelea Soko la Madini Kahama na baadaye itatembelea Nzega. Ziara ya kamati kutembelea masoko imefanywa na kamati hiyo baada ya kutembelea Soko Kuu la Madini Geita na Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.