*******************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya watu wote wakiwemo wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu ambao wanajihusisha na utoroshaji wa madini, waache mara moja, Serikali ipo makini imejidhatiti vya kutosha na kwamba haitokuwa na huruma dhidi yao.
Serikali imefuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT-18%) na kodi ya zuio (withholding tax-5%) kwa wachimbaji watakaouza madini kwenye masoko yalioanzishwa nchini ikiwa ni mikakati ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili waweze kuongeza uzalishaji na hivyo kujiongezea tija na kuchangia katika pato la Taifa.
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumapili, Septemba 22, 2019) wakati akifungua maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayofanyika kwenye uwanja wa CCM Kahangalala mjini Geita. Amesema kwa wale wasiotaka kuelewa na kuacha kutorosha madini Serikali itashughulika nao.
Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto wanazokutana nazo wachimbaji wadogo ikiwemo matumizi ya teknolojia duni katika uchimbaji na uchenjuaji madini. “Nitoe wito kwa wadau kuitumia fursa ya uwekezaji kwa kuanzisha biashara ya vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji nchini.”
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wadau wa madini kuwa katika mkutano wa 16, wa Bunge la 11 lilijadili na kuridhia Azimio la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu kupunguza kwa kadiri iwezekanavyo matumizi ya zebaki ifikapo 2030.
Amesema lengo la mkataba huo ni kuanza kupunguza na hatimaye kuacha matumizi ya zebaki kwenye uchenjuaji wa dhahabu hususan kwa wachimbaji wadogo. Kwa mantiki hiyo, amewasihi wachimbaji wadogo kuepuka matumizi ya zebaki katika uchenjuaji na kuanza kutumia njia nyingine zilizopo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kwa kipindi kirefu kumekuwepo na changamoto ya wachimbaji wadogo kufanya shughuli za uchimbaji bila kuwa na taarifa sahihi za kijiolojia, hivyo kusababisha wachimbaji wengi wadogo kuchimba kwa kubahatisha na hata wengine kutumia imani za kimila katika kuchagua maeneo ya uchimbaji.
“Kwa msingi huo, nawahimiza wadau mbalimbali katika Sekta ya Madini hususan wachimbaji wadogo kuitumia kikamilifu Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili kupata taarifa muhimu na sahihi za kijiolojia pamoja na ushauri wa kitaalamu katika utafutaji wa madini.”
Amesema sambamba na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa kuzingatia taarifa za kijiolojia kupitia GST na STAMICO, Serikali imeendelea kuandaa machapisho yenye kuonesha maeneo yanakopatikana madini nchini.
Waziri Mkuu amewataka wachimbaji wadogo kutumia fursa ya uwepo wa taasisi hiyo ili kuepuka kuwekeza fedha zao nyingi katika maeneo ambayo hayana madini na hivyo, kufanya kazi kwa kubahatisha jambo ambalo halina tija kwao na Serikali kwa ujumla.
Amesema Serikali imeanzisha vituo vya umahiri na vituo vya mfano kwenye baadhi ya maeneo nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya madini kwa wachimbaji wadogo, pia vituo hivyo, vitatumika kufanya maonesho ya madini na vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji madini.
Kaulimbiu ya maonesho hayoinasema ‘Madini ni Chachu ya Ukuaji wa Uchumi wa Viwanda’ Tuwekeze kwenye Teknolojia Bora ya Uzalishaji na Tuyalinde Masoko ya Madini.
Amesema kaulimbiu hiyo inakwenda sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 ambayo pamoja na mambo mengine inaielekeza Serikali kusimamia na kuhakikisha uwekezaji katika shughuli za kuongeza thamani madini ili kukuza mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kwa sasaSerikali na makampuni yanayomiliki migodi wanaheshimiana kwani makampuni hayo yanatii magizo na kufuata sheria za nchi.
Waziri Doto amesema kabla ya kuåfunguliwa kwa masoko ya madini nchini makusanyo ya dhahabu yalikuwa kilo 101 kwa mwezi hivi sasa baada ya masoko kufunguliwa makusanyo yameongezeka na kufikia kilo 1,974.
Hata hivyo, Waziri huyo wa Madini amesema kwa sasa nidhamu ya Watanzaniua katika kusimamia ununuzi na uuzaji dhahabu imevutia wauzaji dhahabu toka nchi za jirani kwani hakuna tena wizi wala utapeli katika biashara hiyo.
Hivyo, Waziri huyo ameyataka makampuni yanayomiliki migodi kutoa tenda kubwa kwa wazawa na makampuni ya ndani badala ya kuyapa makampuni ya nje na kuzipa kampuni za ndani tenda ndogondogo.