Na Mwandishi Wetu
Jeshi laPolisi Visiwani Zanzibar limetakiwa kuwakamata watu wote wanaojihusisha na kushabikia mapenzi ya jinsia moja sambamba na watumiaji wa Dawa za Kulevya ambayo ni matendo yanayoenda kinyume na sheria za nchi sambamba na mila na tamaduni za jamii zetu.
Amri hiyo imetolewa leo Visiwani Zanzibar na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni wakati akigawa vifaa mbalimbali kwa vijana wajasiriamali ili waweze kujiendeleza na shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kuleta maendeleo katika nchi
“Kwenye eneo la changamoto za vijana hasa tunapozungumzia uhalifu unaoathiri maisha yetu hasa ya Visiwa hivi viwili tuna changamoto ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia hasa kwa kina mama na watoto lakini pia tuna changamoto ya dawa ya kulevya, kuna juhudi kubwa sana zimefanywa na Serikali zote mbili katika kudhibiti uhalifu huo” alisema Masauni
“…..Jambo lingine la kusikitisha sana ni kuona vijana wetu wadogo wa kiume wanaharibika na nawaomba wananchi tuwe mabalozi kwa watoto wetu hawa wakiume si suala nzuri sana kwa mustakabali wa nchi hii kuwa ma vijana wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, natoa wito kwa Jeshi la Polisi kuwakamata watu wote wenye desturi ya kushabikia na kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja na hatua kali zichukuliwe juu yao ili kukomesha tabia hiyo” aliongeza Masauni
Akigusia maendeleo ya Teknolojia ya Habari Naibu Waziri Masauni amesema kama nchi imekua ikikabiliwa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na teknolojia ambayo yamepelekea matumizi yasiyo sahihi ya mitandao hali inayopelekea mmomonyoko wa maadili katika jamii tunazoishi.
Wakizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo vijana hao wajasiriamali wameiomba serikali kukamata wanaodaiwa kuwa wafanyabiashara wakubwa wa madawa ya kulevya kwani wamepelekea vijana wengi ambao ni nguvu kazi kupotelea kwenye tabia hatarishi ikiwemo kushiriki mapenzi ya jinsia moja,uvutaji wa bangi na matumizi ya dawa za kulevya.
Vifaa vilivyogaiwa kwa vijana hao ni vyerehani,mashine za kutengenezea juisi ya miwa,mashine za kukaangia chipsi,vifaa mbalimbali vya mafundi makenika na ujenzi, mikokoteni kwa ajili ya Vikundi mbalimbali vya mazingira Visiwani humo ambavyo gharama yake kwa ujumla ni milioni Hamsini.