Muonekano wa nyumba takribani 20 ambazo tayari zimejengwa katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya Maafisa na askari katika Gereza Kuu Isanga zikiwa katika hatua mbalimbali ya ujenzi.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike akisalimiana na Maafisa wa Jeshi la Magereza mkoani Dodoma alipowasili kwenye ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya Maafisa na askari katika Gereza Kuu Isanga, leo Septemba 21, 2019.
Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike(mwenye miwani) akiangalia mbao zinazotumika katika hatua mbalimbali za ujenzi wa mradi wa nyumba za makazi ya Maafisa na askari katika Gereza Kuu Isanga, alipotembelea eneo hilo la ujenzi, leo Septemba 21, 2019. (Picha zote na Jeshi la Magereza).
***************************
Na ASP. Lucas Mboje, Dodoma;
KAMISHNA Jenerali wa Magereza nchini, Phaustine Kasike amekagua ujenzi unaoendelea wa nyumba za makazi ya Maafisa na askari katika Gereza Kuu Isanga ambao unatumia nguvu kazi ya wafungwa wa gereza hilo, jijini Dodoma na ameridhika na kasi ya ujenzi huo.
Akiwa eneo hilo la ujenzi leo(Jumamosi), Kamishna Jenerali Phaustine Kasike ameelezea kufurahishwa, kuridhika na kasi ya hatua mbalimbali za ujenzi ulipofikia na ameupongeza Uongozi wa Magereza mkoani Dodoma kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
“Mmeonesha namna gani mmejipanga vizuri katika kutekeleza Mkakati wa Jeshi katika kutatua uhaba wa makazi ya Maafisa na Askari, hivyo niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya, chapeni kazi,” alisema Kamishna Jenerali Kasike.
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoani Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Keneth Mwambije amemshukru Kamishna Jenerali kwa kutembelea mradi huo na kujionea hatua mbalimbali za ujenzi ikiwemo kuwatia moyo Maofisa, askari na Wafungwa wanaoshiriki kikamilifu katika ujenzi huo.
Aidha, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Keneth Mwambije, amemhakikisha Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza kuwa wataendelea kutekeleza mkakati huo wa ujenzi wa nyumba za tofali za kuchoma ili kuhakikisha kuwa wanatekeleza maelekezo ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama aliyoyatoa kwa Jeshi hilo kuhusu ujenzi wa makazi ya Maafisa na askari kwa kutumia nguvu kazi ya wafungwa waliopo magerezani.
Ujenzi wa nyumba hizo za tofali za kuchoma ulianza rasmi Aprili, 2019 ambapo hadi sasa jumla ya nyumba 20 zimejengwa na zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, moja kati ya nyumba hizo tayari imekwishapauliwa, nyumba tano(05) zimekwisha fungwa lenta na nyingine 14 zinasubilia kufungwa lenta hivi karibuni.