Daktari Bingwa wa Virusi vinavyosababisha Saratani, ambaye pia mtafiti anayefanya tafiti za seli za saratani, Dkt. Kandali Samweli,(wa pili kushoto) akimpatia elimu juu ya upimaji wa homa ini, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi (kulia wa pili), wakati wa upimaji huowa hiari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu ya Tanzania, uliopo jijini Dar es Salaam.
Daktari Bingwa wa Virusi vinavyosababisha Saratani, ambaye pia ni mtafiti anayefanya tafiti za seli za saratani, akitoa ufafanuzi juu ya kipeperushi chenye maelezo kuhusu homa ya Ini.
Baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakisubiri huduma ya upimaji homa ya ini katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu ya Tanzania.
Naibu Msajili, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Augustine Rwizile, akichukuliwa kipimo kwa ajili ya kupima homa ya ini.
Afisa Rasilimali Watu, wa Mahakama Kuu, Bw. Raphael Bonavanje akichukuliwa kipimo kwa ajili ya kupima homa ya ini na Mtaalamu wa Maabara, Bw Costantine Anga kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, iliyopo jijini Dar es Salaam.
Askari Magereza, Nicky Nyandura, wa Gereza la Segerea akichukuliwa kipimo kwa ajili ya kupima homa ya ini.
Mlinzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Naima Mandai akichukuliwa kipimo kupima homa ya ini.
(Picha na Aziza Muhali (SJMC)
……………………
Aziza Muhali- (SJMC)
Imeelezwa kuwa watu walio katika hatari ya kupata maambukizi ya homa ya ini kwa urahisi ni watumiaji wa dawa za kulevya, watoto wadogo na watoa huduma za afya, ambapo wamekuwa wakipewa kipaumbele kupata chanjo ya ugonjwa huo dhidi ya maambukizi.
Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Virusi vinavyosababisha Saratani, ambaye pia ni mtafiti anayefanya tafiti za seli za saratani, Dkt. Kandali Samweli
wakati wa uendeleaji wa zoezi la upimaji homa ya ini kwa hiari, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Alisema kwaupande wa wanawake upimaji huo ni fursa ya kuwakinga watoto, vizazi sasa na vizazi vijavyo.
Dkt. Samweli aliongeza kuwa kupata chanjo ya ugonjwa huo, sio kinga dhidi ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa kuwa Virusi vya Hepatitis B hushambulia ini, wakati VVU huathiri sehemu nyeupe za damu(RNA). Pia alisitiza kwamba watu wanaopata chanjo hiyo, hawatakiwi kunywa pombe mara baada ya chanjo mpaka saa 24 kupita.
Hata hivyo kunaweza kuwa kuna mfanano wa dalili za ugonjwa wa ukimwi na ugonjwa wa ini, ambapo alizitaja dalili za ugonjwa wa homa ya ini ambazo ni ngozi na macho kuwa ya njano pamoja na kuwashwa ngozi, huku akifafanua kwamba dalilihizo hujitokeza mwishoni ambapo mgonjwa anakuwa ameathirika kwa muda mrefu.
“Hakikisheni mnatunza kadi mlizopatiwa wakati wa chanjo ili ziweze kuonyesha mlolongo mzuri wa utoaji wa chanjo hiyo, mpaka mtakapomaliza awamu zote tatu, zikiwemo taarifa zote za afya,” alisema Dkt. Samwel.
Upimaji huo, ulioanza jana ambao umehusisha baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam waliojitokeza kwa hiari, umemalizika leo Septemba 20, mwaka huu.