Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Dkt. Gabriel Mukungu (kulia) akimuelezea Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe Felix Lyaviva (katikati) namna watuhumiwa wa makosa ya barabarani wanaokamwatwa kupitia Mfumo wa Usimamizi wa Makosa Barabarani (TMS) kwanavyotumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Maduhuli ya Serikali (GePG) katika banda la Serikali Na. 26 kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa Sekta ya Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa, unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akifafanua jambo alipokuwa akielezewa namna mifumo ya kielektroniki ya kukusanya maduhuli ya Serikali wa GePG, Mfumo wa Usimamizi wa Makosa Barabarani (TMS) na Mfumo wa Taarifa za Mali zilizopote (Los Report System) inavyofanya kazi ,kutoka kwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Dkt. Gabriel Mukungu katika banda la Serikali Na. 26 kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa Sekta ya Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa, Jijini Dar es Salaam
Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakijiandaa kumpokea Waziri Mkuu, Mhe. Kasim Majaliwa (hayupo pichani) katika banda la Serikali Na. 26 la mifumo ya kielekroniki ya kukusanya maduhuli ya Serikali, Mfumo wa Usimamizi wa Makosa Barabarani (TMS) na Mfumo wa Taarifa za Mali zilizopotea (Los Report System) kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC) wa Sekta ya Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa, Jijini Dar es Salaam.
****************************
Na Farida Ramadhani, WFM, Dar es Salaam
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ametembelea banda la Serikali Na. 26 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) na kujionea namna mifumo ya kielektroniki ya kukusanya maduhuli ya Serikali wa GePG unaosimamiwa na Wizara ya Fedha na mfumo wa Jeshi la Polisi wa kudhibiti wasiolipa faini za barabarani (TMS) inavyofanya kazi.
Waziri Mkuu amefanya tukio hilo kabla ya kufungua rasmi Mkutano wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wa Sekta ya Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa, unaofanyika Jijini Dar es Salaam.
Aliwapongeza wabunifu wa mifumo hiyo ambayo kwa sasa inasaidia Serikali kupata mapato yake kwa wakati pamoja na kupunguza makosa ya barabarani ambayo yamekuwa yakiongeza ajali na kupunguza nguvu kazi ya Taifa.
Alisema uwekezaji katika Sekta ya Tehama ni muhimu kwa nchi wanachama wa SADC ili kudhibiti uhalifu wa mtandaoni pamoja na kusimamia matumizi ya fedha za umma.
Naye Mkuu wa Uendeshaji wa Mfumo wa GePG kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Basil Baligumya, alisema Wizara imeshiriki mkutano huo ili kuzionesha nchi mbalimbali zinazoshiriki mkutano huo namna Tanzania imepiga hatua katika maendeleo ya teknolojia hususani katika usimamizi wa fedha na ukusanyaji mapato ya Serikali kupitia mfumo wa GePG.
Bw. Basil alisema mfumo huo unadhibiti fedha za umma, umeongeza makusanyo na uwazi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, pamoja na kuongeza usahihi wa taarifa za mapato.
“Mfumo huu umerahisisha ulipaji wa huduma mbalimbali za umma na kupunguza gharama nyingi ambazo zilikua zikiambatana na ukusanyaji wa mapato ya Serikali”, alisema.
Alisema kwa kuwa kubadilishana uzoefu ni miongoni mwa malengo ya mkutano huo, wako tayari kujifunza mbinu mpya za kuendeleza mifumo nchini pamoja na kuzielekeza nchi zitazokuwa tayari kujifunza namna ya kutengeneza mifumo ya kusimamia mapato ya nchi zao.
Kwa nyakati tofauti, washiriki mbalimbali waliotembelea banda hilo wameipongeza Serikali kwa kuanzisha mifumo hiyo ambayo itasaidia kudhibiti ubadhilifu wa fedha za umma, kukusanya mapato ya serikali kwa wakati pamoja na kudhibiti makosa ya barabarani.
Washiriki hao wamewapongeza watumishi wote walioshiriki katika kutengeneza mifumo hiyo kwani wameonesha uzalendo wa dhati kwa kuiwezesha Serikali kuweza kisimamia mapato yake kwa wakati.