***********************************
Na Silvia Mchuruza;
Kagera.
Shirika la Wakala wa Meli Tanzania TASAC Mkoa wa Kagera limesema kuanzia sasa litaanza kutoa adhabu kwa abiria wasiovaa maboya na Majaketi ya kujiokolea wawapo kwenye vyombo vya kusafiria majini kwa kuwatoza faini kwa mtu mmoja shilingi laki 5, kumfungia chombo mmiliki, kufikishwa mahakamani na kifungo cha miaka miwili jela au vyote kwa pamoja.
Agizo hilo limetolewa Septemba 19, 2019 na Afisa Mfawidhi na mkaguzi wa vyombo vya Maji mkoani Kagera David Chivagi akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Chivagi amesema changamoto kubwa ni kwa abiria ni kutokubali kuvaa maboya huku manahodha wakiwa hawawaelekezi abiria kuvaa maboya hayo matokeo yake wengine huyalalia, na kuyakalia mwishowe huharibika na kupoteza ubora badala ya kuyavaa kwa ajili ya usalama wa maisha yao.
“Shirika letu limekuwa likitoa elimu kwanza,sasa kinachofuata ni faini. Faini ya shilingi laki 5, kumfungia chombo mmiliki, kufikishwa mahakamani na kifungo cha miaka miwili jela au kupigwa vyote kwa pamoja itakuwa fundisho katika jamii”,amesema Chivagi.
“Utakuta manahodha na wasaidizi wake wanasema boya hili hapa vaa bila kuelekeza namna vizuri namna ya uvaaji.Wapo wanao kataa kuyavaa kabisa wakidai wao ni magwiji katika kuogelea wakati ni kifo” amesema.
Ameeleza kuwa ajali ya hivi karibuni ya boti iliyokuwa imebeba abiria 56 na pamoja na mizigo kuwaka moto ndani ya Ziwa Victoria,abiria wengi walinusurika kutokana na uvaaji wa maboya.
Amesema abiria anatakiwa kupanda katika chombo akiwa umevaa maboya na kwamba kwa yule anayekosa haruhusiwi kusafiri bila vazi hilo na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Amewataka wananchi na wamiliki wa vyombo vya usafiri wanapaswa kufuata sheria za usalama na ulinzi ikiwemo uhifadhi wa mazingira ikiwemo kutotupa vitu hovyo hovyo majini ,kutochafua maji kwa kutomwaga mafuta na oil na kuzingatia usalama kwa watu walionao katika chombo.
Shirika la Wakala wa Meli Tanzania TASAC limeundwa kwa sheria ya Bunge sheria ya nchi no 14 ambapo katika sheria hiyo limepewa maajukumu kadhaa ikiwemo kuhakikisha usalama wa vyombo vya majini, Bandari na Mazingira , kuhakikisha nyaraka za mizigo inayoingia nchini na inayotoka ziko salama na zimekaguliwa lakini pia jukumu la kufanyia ukaguzi mizigo inayoingia na kutoka.