Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa –TAMISEMI,
Mhandisi Joseph Nyamhanga akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo kwa Maafisa Habari na Mwasiliano wa Serikali na taasisi zake leo jijini Dodoma. Mafunzo hayo ya siku tano yaliandaliwa kwa ushirikiano baina ya Idara ya Habari – MAELEZO na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kwa lengo la kuwajengea uwezo maafisa hao. Kutoka kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa TAGCO Bi. Saraha Kibonde Msika na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Bw. Jonas Kamaleki.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo kwa Maafisa Habari na Mwasiliano wa Serikali na
taasisi zake wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa –TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo leo jijini Dodoma. Mafunzo hayo ya siku tano yaliandaliwa kwa ushirikiano baina ya Idara ya Habari – MAELEZO na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kwa lengo la kuwajengea uwezo maafisa hao.
**************************
Na Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma
Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wameahidi kuitangaza miradi mbalimbali na kutomwangusha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli. Wameyasema hayo leo (Ijumaa) wakati wa kufunga mafunzo ya siku tano yaliyolenga kuwanoa katika kuandika kwa usahihi na umakini habari za Serikali.
Akifunga mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga, alimewataka maafisa hao kuitangaza miradi mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa wananchi.
“Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa sana ikiwemo ujenzi wa barabara za lami, madaraja, reli ya kisasa, ujenzi wa vituo vya afya na hospitali, utoaji wa elimu bila malipo, ununuzi wa ndege mpya pamoja na ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere pale Dar es Salaam”.Amesema Mhandisi Nyamhanga.
Amesema, Maafisa Mawasiliano wanalo jukumu la kutangaza miradi hiyo na mingine mingi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Akifungua mafunzo hayo mapema wiki hii, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi aliwaeleza washiriki hao kuwa Rais Magufuli anataka kuona taasisi zote za umma zikitangaza kwa wakati na usahihi majumu waliyopewa kuyafanya.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Afisa Habari wa Halmashauri ya Bahi, Dodoma, Bw. Benton Nollo amesema mafunzo hayo yamekuwa muhimu sana kwao na amemuahidi Rais Rais Magufuli kuwa hawatamwangusha na watatoka Dodoma wakiwa wameiva zaidi na wataboresha utendaji wao.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) kwa kushirikiana na
Idara ya Habari (MAELEZO).