UONGOZI wa Yanga umemteua mwandishi wa Habari za Michezo, Hassan Bumbuli kuwa Afisa Habari na Mawasiliano wa klabu, akichukua nafasi ya Dismas Ten ambaye kwa sasa amepandishwa cheo na kuwa Kaimu Katibu Mkuu.
Taarifa ya Yanga iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu, Ten imesema kwamba Mwenyekiti wa klabu, Dk. Mshindo Msolla kwa kushirikiana na Kamati yake ya Utendaji pamoja na Bumbuli imemteua Antonio Nugaz kuwa Afisa Uhamasishaji.
“Kwa niaba ya wanachama, wapenzi na mashabiki wote, uongozi unawatakia kila la heri kwenye utekelezaji wa majukumu yao,”imesema taarifa hiyo.
Bumbuli aliyeanzia kwenye Uandishi wa magazeti ya Bingwa na Dimba hadi Uhariri na Nugaz, mtangazaji wa Redio Clouds wanakuwa watu wa kwanza kabisa kuajiriwa chini ya uongozi mpya wa klabu ulioingia madarakani Mei 5 mwaka huu.
Pamoja na Mwenyekiti, Dk Msolla aliyepata jumla ya 1,276 dhidi ya 60 tu za Daktari mwenzake, Tiboroha aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo chini ya uongozi uliopita, Frederick Mwakalebela alishinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti kwa kura 1,206 akiwashinda Janneth Mbene (Mbunge) aliyepata kura 61, Titus Osoro kura 17, Yono Kevela kura 31 na Chota Chota kura 12.
Msolla,kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania na Mwakalebela aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walipata ushinsi huo wa kishindo katika uchaguzi uliofanyika Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Osyterbay mjini Dar es Salaam.
Walioshinda nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Hamad Islam aliyepata 1,206, Mhandisi Bahati Faison Mwaseba kura 1,174, Dominick Ikute kura 1,088, Kamugisha Kalokola kura 1,072, Arafat Haji kura 1,024, Salum Ruvila kura 976, Saad Khimji kura 788 na Rodgers Gumbo kura 776.
Uchaguzi huo ulifuatia kujiuzulu kwa viongozi wote waliongia madarakani Juni 11 mwaka 2016, Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wao, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay, Hussein Nyika, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Inspekta Hashim Abdallah.
Pamoja na kuwa kocha wa Taifa Stars, Dk. Msolla pia amewahi kuwa mtumishi wa Serikali kwa nafasi mbalimbali, ikiwemo Ukurugenzi wa Uendelezaji wa Mazao katika Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika wakati wa awamu ya Nne chini ya Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.