Home Mchanganyiko WIZARA YA MAJI IMEONESHA MWAROBAINI WA KUMALIZA CHANGAMOTO YA HUDUMA YA MAJI...

WIZARA YA MAJI IMEONESHA MWAROBAINI WA KUMALIZA CHANGAMOTO YA HUDUMA YA MAJI VIJIJINI

0

Na Ismail Ngayonga

MAELEZO

DAR ES SALAAM

 

MAJI ni hitaji muhimu sana katika uhai wa mwanadamu na viumbe wengine na ndiyo maana Maendeleo ya kiuchumi ya nchi yoyote duniani yawe ya viwanda, kilimo na kadhalika yanategemea maji.

Lengo namba sita la Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2015-2030 linaweka msisitizo wa upatikanaji wa huduma za maji safi na salama na usafi wa mazingira kwa wote ikienda sambamba na ulinzi wa rasilimali za maji na miundombinu ya usambazaji maji.

Wakati mahitaji ya maji yanaongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu na kukua kwa shughuli za kiuchumi na kijamii, maeneo kame yameendelea kuwa kame zaidi na matukio ya mafuriko yanaongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Inaelezwa kuwa zaidi ya watu bilioni 2.1 duniani hawapati maji safi na salama na kati ya hao, watu milioni 844 hawapati huduma za msingi za maji ya kunywa, ambapo kati yao zaidi ya watu milioni 340 wanatoka katika Bara la Afrika.

Hali hiyo inaonesha jitihada zaidi zinahitajika katika kuwekeza na kuendesha mindombinu ya huduma za maji kwa ajili ya kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma za majisafi na usafi wa mazingira ili kuendana na kasi ya mahitaji ya maji na malengo ya nchi na ya Umoja wa Mataifa.

Katika Tanzania mahitaji ya maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama vile majumbani, umwagiliaji, viwanda na mazingira ni wastani wa mita za ujazo bilioni 40 kwa mwaka kati ya mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka zilizopo.

Aidha makadirio yameonesha kuwa mahitaji ya maji yataongezeka kufikia wastani wa mita za ujazo bilioni 57 kwa mwaka ifikapo mwaka 2035 na kutokana na mwenendo wa kuongezeka kwa mahitaji ya maji nchini, Serikali imeimarisha ulinzi wa rasilimali za maji ili kulifanya Taifa lisikumbwe na uhaba wa maji katika siku za usoni katika maeneo ya mijini na vijijini.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa anasema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza miradi ya maji mijini na vijijini kwa kujenga miradi mipya, kukarabati na kupanua miradi iliyopo kwa kutumia vyanzo vya maji vya visima virefu na vifupi, mabwawa, chemchemi, mito na maziwa.

Prof. Mbarawa anasema katika kipindi cha mwezi Julai 2018 hadi mwezi Desemba 2018, jumla ya miradi 198 yenye vituo vya kuchotea maji 4,719 imekamilika na kuwanufaisha wananchi wapatao 1,252,731 waishio vijijini na miradi 653 inaendelea kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Waziri Mbarawa anasema Serikali inaendelea na ujenzi wa miradi ya maji vijijini pamoja na kutekeleza programu mbalimbali za kuimarisha uendeshaji na matengenezo ya miradi hiyo ili iwe endelevu ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maji katika vijiji 77 iliyofikia katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

“Katika mwaka 2018/2019, Serikali kwa kushirikiana na BADEA, OFID, Saudi Fund na Kuwait Fund inatekeleza mradi wa maji Same-Mwanga–Korogwe wenye lengo la kuwapatia huduma ya maji wakazi wa miji ya Same na Mwanga, pamoja na vijiji 38 vilivyopo kandokando ya bomba kuu katika Wilaya za Same, Mwanga na Korogwe” anasema Waziri Mbarawa.

Anaongeza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusu ujenzi wa miundombinu ya uzalishaji maji pamoja na miundombinu ya kusambaza maji katika miji ya Same, Mwanga na vijiji tisa vilivyopo kandokando ya bomba kuu na awamu ya pili itahusu kusambaza maji katika vijiji 29 vilivyobaki ambapo Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa awamu hiyo.

Akifafanua zaidi Prof. Mbarawa anaongeza kuwa awamu ya kwanza ya mradi umegawanywa katika vipande vinne,  kipande cha kwanza kilichogharimu Dola za Marekani Milioni 41.36 kinahusu ujenzi wa miundombinu ya kuzalisha maji, ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji hadi kwenye tanki la kuhifadhia maji, mtambo wa kusafisha maji pamoja na ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji.

Prof. Mbarawa anasema kuwa Serikali pia inatekeleza utekelezaji wa mradi wa maji wa Masoko uliopo Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya ambao unahusisha ulazaji wa mtandao wa mabomba, ujenzi 50 wa vidakio vya maji, matanki ya maji na vituo vya kuchotea maji. Hatua za utekelezaji wa mradi zimegawanyika katika vipande vitano.

“Mradi wa maji Masoko utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 wanaoishi katika vijiji vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa, Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga”.

Aidha Ppof. Mbarawa anasema mradi wa maji wa vijiji 100 vilivyopo kandokando ya bomba kuu la maji kutoka Ziwa Victoria hadi miji ya Kahama na Shinyanga unaendelea kutekelezwa chini ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Kahama – Shinyanga (KASHWASA), ambapo wamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo itahusisha vijiji 40 ambapo vijiji 33 vimefanyiwa usanifu.

Anaongeza kuwa kati ya vijiji vilivyofanyiwa usanifu, ujenzi wa miradi kwenye vijiji 14 umekamilika na kunufaisha wananchi wapatao 38,348. Vijiji hivyo ni Runele, Gatuli, Nyashimbi, Magobeko, Kakulu, Butegwa, Nyang’homango, Ng’homango, Jimondoli, Kadoto, Lyabusalu, Mwajiji, Ichongo na Bukamba.

Kuhusu mradi wa maji wa Chiwambo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi uliogharimu Shilingi bilioni 4.49,  ulikamilika mwezi Mei, 2018 ambapo unahudumia vijiji vijiji 30 vilivyopo Kata za Lulindi, Lupumbulu, Namalenga, Chiungutwa, Sindano, Mchauru na Mbuyuni na utekelezaji wa mradi huo ulihusisha ukarabati wa matanki na miundombinu ya maji iliyochakaa, ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji.

Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa anasema Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI iliunda Timu ya Wataalam kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu wa kina wa mradi wa maji Ntomoko uliopo katika vijiji vya Ntomoko-Fai na Makirinya Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma pamoja na vijiji vya Kinkima na Lusangi vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chemba.

Anasema ili kuteleza mradi huo mwezi Februari mwaka huu, Serikali ilisaini mkataba wenye thamani ya Tsh Bilioni 2.27 na Mkandarasi tayari ameanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo ikiwa na pamoja na ujenzi wa matanki matatu, ununuzi wa pampu, ulazaji wa mabomba ya kusafirisha maji pamoja na ujenzi wa chemba.

Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo itihada zaidi zinahitajika katika kuwekeza na kuendesha mindombinu ya huduma za maji kwa ajili ya kuongeza idadi ya watu wanaopata huduma za majisafi nchini.