Na.Alex Sonna,Dodoma
Katika kukabiliana na tatizo la wafanyakazi wa makampuni ya kibiashara nchini kukabiliwa na changamoto ya kutopewa nakala za mikataba ya ajira, kituo cha sheria na haki za binadamu(LHRC) kimeandaa mdahalo wa kitaifa juu ya haki za binadamu na biashara kujadili na namna ya kutatua changamoto hizo.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2017 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC), ilionesha kuwa asilimia 74 ya wafanyakazi wana mikataba lakini baadhi hawapewi nakala huku asilimia 26 hawana kabisa mikataba.
Mdahalo huo umefanyika Jijini Dodoma, na kujumuisha mashirika na wadau mbalimbali, wakati wa kuwasilisha mada, Paul Mikongoti, kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) amesema dhana ya haki za binadamu na biashara ni pana na hali halisi ilivyo nchini, na hasa katika mikataba ya ujira katika makampuni mbalimbali.
Amesema maeneo ambayo yameonekana kuwa na matatizo katika utekelezaji wa masuala la haki za binadamu na biashara kuwa ni maeneo ya makazini, ardhi, mazingira na masuala ya kodi.
“Utoaji wa mikataba imeimarika lakini wengi hawapewi nakala za mikataba, wengine mikataba haikidhi vigezo na hasa kwenye makampuni haya ya kichina yana changamoto sana,”amesema.
Aidha amebainisha kuwa asilimia 95 ya wafanyakazi wanaondoka kazini baada ya muda wa kazi huku asilimia tano wao wakishindwa kuondoka baada ya muda huo uliopangwa.
Kuhusu mafunzo ya afya mahala pa kazi, Ngongoti amesema asilimia 55 ya wafanyakazi wamepewa mafunzo hayo huku asilimia 45 wakiwa hawana elimu hiyo, pia elimu ya sheria ya kazi wanaojua ni asilimia 23 huku asilimia 77 wana uelewa mdogo na wengine hawana kabisa.
Akizungumzia suala la fidia ya ardhi inayochukuliwa kwa ajili ya uwekezaji, Mtoa mada huyo alisema asilimia 42 ya wananchi hawana uhakikika na fidia inayolipwa huku asilimia 64 wanadai kuwa wawekezaji wamekuwa hawaruhusu maeneo yao kutumiwa na wananchi.
Amesema makampuni hayo yana wajibu mkubwa wa kulinda na kusimamia haki za binadamu katika maeneo yake kwa kujibu wa matakwa ya kidunia masuala ya haki za binadamu na biashara ambayo yamewekewa utaratibu ili kutosababisha athari zozote za kibinadamu.
“Suala la kulinda haki za binadamu hakuepukiki, hata kampuni inapokuja kufanya kazi Tanzania lazima ifuate huo utaratibu wa kidunia,”amesema