****************************
Na Silvia Mchuruza;
Kagera;
MKUU wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewasusia kikao watendaji wa mitaa na Kata wa Manispaa ya Bukoba kwa kile alichodai kuwa wameshindwa kuitikia wito wake.
Katika kikao hicho kilichotakiwa kufanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Bukoba saa 7.30 (jana), Gaguti alisema idadi ya watendaji waliojitokeza ni nusu ya watendaji waliopo katika Manispaa ya Bukoba hivyo inaonyesha kuwa watendaji ambao hawakufika wamezarau wito wake.
“Hii ni asilimia 50 ya watendaji wote walioko Manispaa ya Bukoba, ina maana wengine wamezarau wito wangu, nishaurini niwachukulie hatua gani kwa kuzarau wito wangu siwezi kuendelea na kikao hiki ambacho kilikuwa na ajenda mbili muhimu ila nahitaji wale wote ambao hawakufika wachukuliwe hatua za kinidhamu,” alisema.
Pia Gaguti alihoji watendaji waliofika kuwa “kama nimewaita siku ya kazi na hamkufika je itakuwaje nikiwaita siku ya Jumamosi?
Baada ya agizo hilo, Katibu Tawala wa Manispaa ya Bukoba, Kadole Kilungala aliagiza watendaji waliokuwa wamefika waandike majina yao na wale ambao hawakufika waambiwe wafike tarehe 18 (leo) saa 12 asubuhi ofisini kwake.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi, wa Manispaa ya Bukoba, Richard Mihayo, Manispaa ya Bukoba inao watendaji wa kata 14 na wa mitaa 66, wakati waliojitokeza kuhudhuria kikao hicho walikuwa 33.