Home Mchanganyiko NAIBU WAZIRI ULEGA ATOA MIEZI MITATU KUONDOLEWA CHANGAMOTO ZA SOKO LA NYAMA...

NAIBU WAZIRI ULEGA ATOA MIEZI MITATU KUONDOLEWA CHANGAMOTO ZA SOKO LA NYAMA NJE YA NCHI

0

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti mara baada ya kuwasili ofisini kwake kuanza ziara ya kanda ya ziwa.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akipewa maelezo ya ranchi za Mabale, Kagoma na Kikulula zilizopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera na Kaimu Meneja Mkuu wa NARCO Prof. Phillemon Wambura.

***********************************

Serikali imesema itahakikisha katika kipindi cha miezi mitatu ijayo changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi kwenye soko la nyama nje ya nchi zinatatuliwa ili kuhakikisha wafugaji wananufaika kupitia mifugo yao kupitia soko la nje ya nchi.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo katika Ranchi ya Kikulula iliyopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera wakati akizungumza na wawekezaji waliopatiwa vitalu katika ranchi hiyo, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani humo, ambapo amesema baadhi ya masoko nje ya nchi hushindwa kununua nyama kutoka Tanzania kwa madai yasiyo sahihi kuwa mifugo iliyopo nchini ina maradhi.

Akizungumza na wawekezaji takriban 33 waliopewa vitalu katika ranchi ya Kikulula iliyopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, Naibu Waziri Ulega amesema katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ni lazima vikwazo vilivyopo katika soko la nyama nje ya nchi viwe vimetatuliwa kwa wawekezaji kwenye vitalu kuwa na mipango maalum ya ufugaji ili wakaguzi kutoka nje ya nchi wakija kukagua ubora wa mifugo nchini wapate taarifa sahihi itakayowezesha mifugo na nyama itokanayo na mifugo hiyo ipate soko nje ya nchi kwa kuwa na afya bora.

 

Aidha Waziri Ulega amesema Ranchi ya Kikulula lazima iendelezwe na kuwa ya mfano kwa kuwekewa mikakati mbalimbali ili iweze kuwa na tija kwa mfugaji na taifa kwa ujumla pamoja na kuwataka wawekezaji kuendeleza vitalu vyao kwa kuweka miundombinu imara bila kuwa na hofu ya uwepo wa mkataba wa muda mfupi wa mwaka mmoja.

 

Nao baadhi ya wawekezaji katika Ranchi ya Kikukula wameiomba serikali kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo ya ufinyu wa maeneo ya mifugo yao huku wakiipongeza kwa namna inavyoboresha sekta ya mifugo nchini.

 

Kwa upande wake Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO) Prof. Phillemon Wambura akijibu hoja hizo amewataka wawekezaji kuhakikisha wanapata vitalu kwa misingi ya kisheria.

 

Awali Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega mara baada ya kuwasili mjini Bukoba alipata nafasi ya kukutana na mkuu wa mkoa huo brigedia jenerali Marco Gaguti ambapo ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kufanya utafiti namna wafanyabiashara wanavyoweza kunufaika na mabaki ya samaki yakiwemo mabondo.

 

Naibu Waziri Ulega yupo Mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo katika siku ya kwanza ametembelea ranchi za Kikulula na Mabale pamoja na kuzungumza na wawekezaji katika ranchi hizo na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Katanda kilichopo Kata ya Kihanga, Wilayani Karagwe.