*******************************
Na Ismail Ngayonga,
MAELEZO
DAR ES SALAAM
18.9.2019
UKUSANYAJI wa mapato ni moja ya vipaumbele muhimu vya Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea na kupunguza kwa kadri inavyowezekana utegemezi kutoka kwa Wadau wa Maendeleo.
Aidha, azma ya Serikali ya kuifanya Tanzania nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, haiwezi kufikiwa endapo Serikali haitokuwa na uwezo wa kifedha wa kugharamia shughuli mbali mbali za maendeleo.
Takwimu zilizopo zinaonesha tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani mwaka 2015, kumekuwepo na ongezeko la makusanyo kwa mwezi kutoka Tsh Bilioni 800 hadi kufikia Tsh Trilioni 1.3 kwa mwezi kutokana na mwitikio chanya wa wananchi wa kulipa kodi na usimamizi makini katika ukusanyaji mapato.
Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inatekeleza Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 unaozingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya Pili wa Mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 na Agenda ya Dunia ya Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Mwaka 2030.
Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu, Mikoa na Halmashauri iliidhinishiwa jumla ya Tsh Trilioni 6.58 kwa ajili ya Mishahara, Matumizi Mengineyo na Miradi ya Maendeleo, ambapo Kati ya fedha hizo, Tsh trilioni 4.13 ni Mishahara, Tsh Bilioni 649.3 ni Matumizi Mengineyo na Tsh trilioni 1.80 ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.
Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi, kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo anasema katika mwaka 2018/19, Halmashauri Halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 735.6 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya ndani.
Waziri Jafo anasema hadi kufikia Februari, 2019, Halmashauri zilikuwa zimekusanya jumla ya Tsh Bilioni 392.90 sawa na asilimia 53 ya makadirio, ambacho ni sawa na ongezeko la Tsh Bilioni 111.6 ikilinganishwa na kiasi cha Tsh Bilioni 281.3 zilizokusanywa hadi Februari, 2018.
“Ongezeko la makusanyo limechangiwa na kuimarishwa kwa usimamizi na udhibiti, elimu na hamasa kwa walipa kodi na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato pamoja na mkakati uliowekwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI wa kuzishindanisha Halmashauri kila robo mwaka” anasema Waziri Jafo.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo anasema kutokana na mageuzi hayo ya ukusanyaji mapato Ofisi ya Rais TAMISEMI imeendelea kutekeleza vyema mpango wa utoaji huduma bora za afya na kuharakisha Maendeleo ya wananchi kwa kuwa na Hospitali kila Wilaya, Kituo cha Afya kila Kata na Zahanati kila Kijiji.
Akizungumzia kuhusu Mpango wa Maboresho ya Huduma za Afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Waziri Jafo anasema katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, ziliidhinishwa jumla ya shilingi bilioni 100.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali 67 za Halmashauri.
Anaongeza kuwa Hadi Februari 2019, fedha zote zilikuwa zimepokelewa kwenye Halmashauri na ujenzi unaendelea kwa kutumia utaratibu wa “Force Account” kwa kuzingatia Kanuni ya 167 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2013 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016.
Kuhusu hospitali za Halmashauri, Waziri Jafo anasema ujenzi unahusisha majengo saba ambayo yamejengwa kwa kutumia shilingi bilioni 1.5 kwa kila Halmashauri zilizowekwa kwa kila Halmashauri. Majengo hayo ni ya Utawala, majengo ya nje, stoo ya madawa, maabara, jengo la mionzi, jengo la kufulia na jengo la wazazi.
Akifafanua zaidi Waziri Jafo anasema katika mwaka wa fedha 2018/2019, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeendelea na ujenzi, ukarabati na ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma afya 352 ikihusisha ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto, nyumba moja ya mtumishi, jengo la wagonjwa wa nje na chumba cha kuhifadhia maiti.
“Serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa kutumia utaratibu wa “Force Account” ambapo gharama zimepungua kutoka Shilingi bilioni 2.5 hadi Tsh Milioni 400 au 500 kwa kila Kituo cha Afya na Serikali pia metoa jumla ya Shilingi bilioni 41.6 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba sambamba na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa usingizi zaidi ya 200 kwa ajili ya kuimarisha huduma na upasuaji kwenye vituo vya afya” anasema Waziri Jafo.
Waziri Jafo anasema katika kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeratibu uanzishwaji wa Mfumo wa Mshitiri katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara ikiwa ni utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya na kuviwezesha vituo vya kutolea huduma ya afya kupata mahitaji ya vifaa, vifaa tiba, dawa na vitendanishi kutoka kwa wauzaji binafsi walioteuliwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
lengo la Serikali kuhakikisha kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaendelea kutumia fursa za kimapato zilizopo katika maeneo yao na hivyo kutoa huduma bora zaidi na zenye uhakika kwa wananchi.
Ni jukumu la Mamlaka za Serikali za Mitaa kubuni na kuandaa kwa umakini na utaalamu miradi ambayo inatarajiwa kuongeza uwezo wa Halmashauri kimapato ili kuweza kujitegemea na kuboresha utoaji wa huduma bora na zenye uhakika kwa wananchi.