Mkurugenzi wa ESAP, Joel Katala,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kumaliza mdahalo wa kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi pamoja na ndoa za utotoni
Na.Alex Sonna,Dodoma
Wadau mbalimbali wameiomba Serikali kuitazama upya sheria ya adhabu kwa watu wanaowapa mimba watoto isiishie kuwafunga jela miaka 30 watu wanaobainika kufanya makossa hayo, bali iende mbali zaidi hata kwa wazazi ambao watachangia kuwaficha watuhumiwa.
Hayo yalisemwa katika mdahalo wa kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi, ikiwemo mimba na ndoa za utotoni uliyoandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya ESAP Tanzania.
Mkurugenzi wa ESAP, Joel Katala, aliisema katika tafiti mbalimbali zilizofanywa na shirika hilo , imebainika kuwa kuna baadhi ya wazazi wameonekana kuwasaidia watuhumiwa kukimbia kwa kuhongwa fedha kidogo.
Alisema mbali ya kusaidia watuhumiwa kukwepa mkono wa sharia baadhi ya wazazi baadaye baada ya kuona jambo limepoa huruhusu mtuhumiwa kuendelea na maisha ya ndoa na binti yao aliyepewa mimba na kukatisha masomo.
“Naiomba serikali iiangalie upya sheria na itoe adhabu ya miaka thelathini kwa wazazi watakao bainika kutenda kosa la kusaidia mtuhumiwa ili kukomesha kabisa tatizo hilo,” alisema Katala.
Aidha aliwataka wadau na taasisi mbalimbali kushirikiana kwa pamoja ili kuongeza nguvu ya kyitatua changamoto hii badala ya kuiachia serikali pekee.
Kwa upande wake,mmoja wa askari polisi kutoka katika dawati la jinsia katika jeshi la polisi Wilaya ya Dodoma mjini,Amina Mzee, alisema wanakutana na changamoto kubwa za wazazi kutotoa ushirikiano mara baada ya matukio hayo kutoka.
Alisema wakati mwingine wazazi huwalazimisha watoto wao kusema kuwa hawawajui watumiwa hali ambayo uwapa wakati mgumu polisi.
Naye, Ester Suleimani, akizungumza kwa niaba ya wazazi ambao waliudhuria kwenye mdahalo huo, alisema hata wao upata wakati mgumu kukabiliana na changamoto hiyo kwakuwa watoto hawatoi ushirikiano.
Katika mdahalo huo mambo mazito yaliibuliwa ikiwemo la baadhi ya watoto wa kike kudaiwa kufanya mapenzi kinyume cha maumbile kama njia ya kuepukana na changamoto ya mimba za utotoni.
Hayo yaliibuliwa na Mkuu wa idara ya Maendeleo ya jamii halmashauri ya jiji la Dodoma Sharifa Nabalang’anya wakati akieleza namna idara yake inavyopambana na changamoto hiyo.
Nabalang’anya aliwalaumu wazazi kwa kushindwa kuwasimamia na kuwakagua watoto wao mara wanapotoka shuleni na kukagua kazi za ziada za shule pekee bila kujua nyendo zao.
“Wazazi wako bize na shughuli zao hawajui kuwa watoto wao Mara baada ya kutoka shule na siku za wikiendi uenda katika vibanda umiza kuangalia sinema tofauti tofauti ikiwemo sinema za mapenzi Na kujifunza mambo yasiyofaa ikiwemo mapenzi kinyume cha maumbile,” alisema Nabalang”anya.