Serikali imesema kuwa haiwezi kukamilika kila mahitaji yanayotakiwa kwa jamii badala yake wenye uwezi wanatakiwa kusaidia ili kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Wito huo umetolewa jana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana Anthony Mavunde wakati akipokea msaada wa mifuko 100 ya saruji kutoka kwa kampuni ya Camel Cement ili kusaidia ujenzi wa zahanati na vyumba vya madarasa.
Mavunde alisema suala la kusubiri kwamba serikali inaweza kufanya kila jambo si wakati wake badala yake kila mtu mwenye kuweza kufanya jambo lolote hata kama lingekuwa ni dogo anatakiwa kulifanya kwa maendeleo ya taifa.
Alisema pamoja na maendeleo makubwa ambayo nchi inaendelea kupiga hatua, lakini mchango wa sekta binafsi na hata kwamtu mmoja mmoja bado unahitajika ili kusaidiana na serikali.
“Leo nimepokea mifuko hii na ninaahidi kuipeleka kwa walengwa hasa katika shule ya Msingi Mayeto na Zahanati ya Chigongwe, lakini narudia kuwa wanasiasa pekee na serikali hatuwezi kuifanya Tanzania ikasonga mbele katika maendeleo bali wadau wengine wajikoteze,” alisema Mavunde.
Akizungumzia miradi ya maendeleo jimboni kwake mbunge huyo wa Dodoma Mjini alisema bado kuna changamoto za upungufu wa vyumba vya madarasa kutokana na ongezeko la wanafunzi kupitia mpango wa elimu bila malipo hivyo akaomba makampuni na wadau wengine kufanya kama kilichofanyika na kampuni ya Camel Cement.
Ofisa masoko wa kampuni hiyo Karim Hassan alisema mifuko waliyoitoa kwa jimbo la Dodoma ni sehemu ya faida wanayopata kutokana na mauzo ya bidhaa zao hivyo wanaamua kurudisha fadhira kwa jamii yenye uhitaji.
Hassan alisema kampuni hiyo imeamua uweka mizizi yake Jijini Dodoma kwa kuzingatia kuwa ndiyo makao makuu ya nchi na hivyo unahitaji kujengwa kwa kasi zaidi.
Mmoja wa wanakijiji wa Chigongwe Ayub Nhonya alisema alisema msaada huo waliusubiri kwa muda mrefu kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa zahanati yao kutokana na umabli mrefu wa kufuata huduma hiyo ambao wamekuwa wakiupata.