Baadhi ya mabehewa yaliyowasili Katavi
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Lilian Charles Matinga akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara waliokuwepo stesheni hapo
……………………
Kufuatia malalamiko mbalimbali ya wafanyabiashara wasafirishaji wa mazao kushindwa kusafirisha mizigo yao kutokana na uhaba wa mabehewa, Shirika la Reli Tanzania limepeleka mabehewa 40 ya mizigo mkoani katavi
Mabehewa hayo yatasaidia kuondoa shehena ya mazao iliyokuwa imerundikana katika stesheni ya reli ya Mpanda
Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Reli Tanzania; bwana Focus Sahani akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi mkuu shirika hilo amesema mabehewa mengine yataendelea kuja mpaka zoezi la utoaji mazao litakapokamilika
Amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Dkt. John Pombe Magufuli imetoa mabehewa hayo katika maeneo mengine kutokana na uhitaji uliopo sasa Mpanda
Ameongeza kuwa watasimamia zoezi zima la upakiaji mizigo ambalo linadaiwa kukumbwa na rushwa
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara wanaosubiri mazao yao kusafirishwa wamelalamikia hali ya urasimu katika upatikanaji wa mabehewa ambapo wamedai kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakishikilia mabehewa bila hata ya kuwa na mizigo
Aidha kutokana na hali hiyo wameiomba serikali kubadilisha utaratibu na kulipia kwanza mabehewa kuliko kuyatoa kwa walanguzi
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi; Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Lilian Matinga amesema katika mabehewa yaliyofika, mabehewa kumi yatatengwa kwa ajili ya kubeba pamba na 30 yatabeba mazao mengine
Ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kuepusha pamba kuharibika pindi itakaponyeshewa na mvua