Waziri wa Madini akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wafanyabiashara, watoa huduma na uongozi wa Mgodi wa Dhabau wa Geita (GGM) mjini Geita.
Sehemu ya Washiriki wa mkutano baina ya wafanya biashara, watoa huduma na Uongozi wa Mgodi wa Dhabau wa Geita (GGM) mjini Geita.
Waziri wa Madini akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mha. Robert Gabriel baada ya kufungua mkutano wa wafanya biashara, watoa huduma na uongozi wa Mgodi wa Dhabau wa Geita (GGM) mjini Geita.
…………………
Na Issa Mtuwa – Geita
Pamoja na kuupongeza Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) katika masuala ya ulipaji kodi, utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa jamii (CSR) na kuwa mgodi namba moja nchini kwa utekelezaji wa Sheria za Madini, bado serikali hairidhishwi na namna mgodi huo na mingine inavyowashirikisha wananchi moja kwa moja.
Kauli hiyo ilitolewa Septemba 16 na Waziri wa Madini Doto Biteko mjini Geita kwenye mkutano uliowakutanisha wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali mkoani Geita , wananchi na uongozi wa GGM. Mkutano huo uliokuwa na lengo la kufahamishana fursa za kibiashara na utoaji huduma zilizopo kwenye mgodi wa GGM.
“Naomba niwe mkweli, mgodi wa GGM ni wakwanza hapa nchini katika ulipaji wa kodi, utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii (CSR) lakini sijaridhishwa na namna ambavyo mgodi unavyo washirikisha wananchi moja kwa moja ili waone umaana wa uwepo wa raslimali hii katika mazingira yao,” alisema Biteko.
Aliongeza kuwa, ni wajibu wa GGM kuwaeleza wananchi fursa zilizopo na namna mgodi unavyowashirikisha ili madini yanapokwisha wananchi wabaki na kumbukumbu ya uwepo wa dhahabu hapa mkoani humo.
Pia, Waziri Biteko alitaka baada ya mkutano huo kuwe na maazimio yatakayo ratibiwa na kusimamiwa na Mkuu wa Mkoa huku akisisitiza maazimio hayo kueleza namna mgodi huo unavyokwenda mkieleza namna mnavyokwenda kuwahusisha wananchi.
Kwa upande mwingine, Waziri Biteko amekemea vikali vitendo vya udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watu wanaopewa fursa ya kufanya biashara na migodi na kueleza kwamba, amekuwa akipokea malalmiko ya udanganyifu na wizi kwenye migodi unaofanywa na baadhi ya wasio wema na amewataka kubadilika na kutenda haki ili kuongeza imani ya kuendelea kuwatumia watoa huduma wa ndani.
Waziri Biteko alisema kuanzia sasa Kamishna Msaidizi anaye shugulikia masuala ya Ushiriki wa Nchi na Wananchi katika Sekta ya Madini (Local Content) kutoka ofisi ya Kamishna wa Madini atakuwa anapita kukagua namna utekelezaji wa masuala ya Local content yanavyo tekelezwa na hii sio kwa mgodi wa GGM peke yake bali kwa migodi yote hapa nchini.
Pamoja na kuelezwa kuwa mpaka sasa mgodi wa GGM una asilimia 97 ya wafanyakazi ni wazawa, bado haitakuwa na maana kama maamuzi ya mambo mbalimbali yatakuwa yanasubiri asilimia 3 ya wafanyakazi wanaotoka nje.
Halikadhalika, Waziri Biteko aliwakumbusha watendaji wote wa Wizara ya Madini na Taasisi zake zote kuhusu agizo alilolitoa akiwa ziarani Mkoani Lindi wiki mbili zilizopita kuendelea kufuatilia yanayojiri kwenye ziara zake hususani viongozi kwani patafika mahali wananchi na wadau watatakiwa kupatiwa majibu ya papohapo ili kuondokana na kero bila kusubiri muda mrefu. Hivyo, alimtaka kila mtendaji kuwa tayari kupokea simu pindi atakapo muhitaji na kutolea majibu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel alisema bado kwenye mgodi wa GGM kuna “figisu figisu” katika kuwapatia ajira wana Geita kwa visingizo mbalimbali na hususan ujuzi wa lugha ya Kiingereza na kuwataka kubadilika katika hilo.
“Kuna figisu figisu ya utoaji wa ajira pale mgodini, moja ya sababu mnasema lugha, hicho Kiingereza sio ndio kinachofanya kazi, hiyo lugha sioni ulazima wake na sio wakati wote watakuwa wanaongea muda mwingi ni wakufanya kazi wakiwa wenyewe hata kisukuma watakuwa wanaimizana kufanya kazi,” alisema Mhandisi Gabrile.
Naye. Meneja Mkuu wa Mgodi wa GGM Richard Jordinson alisema kama mgodi wamedhamiria kuifanya jamii ya Geita kuwa sehemu ya mgodi na ndiyo sababu tayari wamewisha sainishana mikataba mbalimbali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Na kuongeza, ni dhamira yao kuiona Geita yenye dhahabu inakuwa na nuru ya dhahabu na wako tayari kushirikiana na jamii na serikali, kutii mamlaka za serikali na kufuata marekebisho yote yaliyofanywa kwenye sheria ya madini na ndio maana wameamua kukutana na wadau ili wajadili masuala yote.
Aidha, Uongozi wa GGM umemshukuru Waziri Biteko na wafanyakazi wote wa wizara kwa ushirikiano wanao upata mara kwa mara kwani wanaifanya kazi yao kuwa rahisi, mara zote wamekuwa wakijadiliana na kukubaliana katika masuala mbalimbali.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Anglo Gold Ashanti Bara la Afrika, Sicelo Ntuli alisema mgodi GGM mwaka 2018 ulitenga bilioni 9.2 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa mkoa wa Geita peke yake na wanatarajia kuanza kutekeleza miradi hiyo mwaka wa fedha wa 2019/20.