Alex Msama Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promosheni akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake Kinondoni jijini Dar es salaam wakati alipoelezea kusikitiswa kwake na suala zima la kutopewa nafasi kuutumia uwanja wa Taifa kwa ajili ya Tamasha la Pasaka.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Bw Alex Msama Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promosheni wakati akizungumza nao leo ofisini kwake Kinondoni jijini Dar es salaam.
………………………………………………
Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promosheni ya jijini Dar es salaam inayoandaa matamasha ya muziki wa injili Tamasha la Pasaka na Tamasha la Krismass Bw. Alex Msama amesema anasitisha kwa muda uandaaji wa matamasha hayo katika jiji la Dar es salaam.
Msama amesema amechukua uamuzi huo kutokana na kunyimwa kibali cha kuutumia uwanja wa taifa unaomilikiwa na serikali kwa muda wa miaka mitatu sasa.
Ameongeza kwamba Tangu mwaka 2017-2019 wamekuwa wakiandika barua kwenda wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuomba kuutmia uwanja huo bila mafanikio kwakuwa barua zote ambazo walizituma hazijawahi kujibiwa.
Ameongeza kwamba Tamasha la Pasaka linachukua zaidi wa watazamaji 45,000 watu ambao ni wengi sana hivyo maeneo mengine hayawezi kutosheleza zaidi ya uwanja wa Taifa au uwanja wa Uhuru.
Fullshangweblog ilipowasiliana na Waziri wa habari utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kwa njia ya simu alisema wizara ya habari ni kubwa na ina mambo mengi, Hivyo yeye hana taarifa hizo, lakini pia mtu ambaye anapokea barua zote za wizara ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo hivyo mnaweza kuwasiliana naye ili kupata majibu kamili kuhusu taarifa hizo,Juhudi za kumtafuta Katibu Mkuu zinaendelea.