Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula akipongezwa na mkazi wa Kata ya Komolo baada ya kuzindua madarasa matatu ya shule ya msingi Nadoilchukin yaliyojengwa na shirika la ECLAT Foundation kwa gharama ya shilingi milioni 134.
Mwenyekiti wa shirika la ECLAT Foundation Peter Kiroiya Toima, akinyanyua juu hati ya pongezi ya kuthamini mchango wake kwa jamii iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula, baada ya kuikabidhi serikali madarasa matatu ya shule ya msingi Nadoilchukin kwa gharama ya shilingi milioni 134.
Ofisa miradi wa shirika la ECLAT Foundation, Bakiri Angalia na Katibu wa chama cha walimu nchini (CWT) Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Nazama Tarimo wakisoma kibao cha uzinduzi wa madarasa matatu ya shule ya msingi Nadoilchukin yaliyojengwa na ECLAT Foundation kwa gharama ya shilingi milioni 134.
…………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
JAMII ya wafugaji wa Kata ya Komolo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, imetakiwa kutumia fursa ya uwepo wa shule ya msingi Nadoilchukin iliyojengwa na shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Foundation kwa kuwapatia watoto wao elimu na siyo kuwafanya wachungi wa mifugo.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula ameyasema hayo wakati akikabidhiwa madarasa matatu ya shule ya msingi Nadoilchukin yaliyojengwa na shirika la ECLAT Foundation kwa gharama ya shilingi milioni 134.
Mhandisi Chaula alisema jamii ya eneo hilo haina kisingizio cha ukosefu wa shule hivyo kuwachungisha mifugo watoto wao au kuwaozesha kwani kuna shule ambayo ipo karibu kwa hiyo wawasomeshe.
Alisema mdau wa maendeleo Peter Toima ambaye ni Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la ECLAT Foundation anapaswa kupongezwa kwa kuwajali wananchi wa eneo hilo hadi kujenga na kukarabati shule hiyo.
“Mimi huwa namwita Mwenyekiti wa ECLAT Foundation Peter Toima kuwa ni bwana maendeleo kutokana na tamaa yake ya kuona wananchi wa eneo hilo wanapata maendeleo kupitia sekta mbalimbali,” alisema Chaula.
Ofisa miradi wa shirika la ECLAT Foundation, Bakiri Angalia alisema wametumia shilingi milioni 134 kwenye shule hiyo kwa ufadhili wa shirika la Upendo Society la nchini Ujerumani.
Angalia alisema kwenye shule hiyo wamejenga madarasa matatu, wamekabidhi madawati 69 na kuweka mfumo wa uvunaji wa maji ya mvua.
Alisema awamu ya pili ya ujenzi wa shule hiyo watafanya ukarabati kwenye majengo chakavu hivi karibuni.
Mwenyekiti wa shirika la ECLAT Foundation, Peter Toima alisema wataendelea kushirikiana na serikali katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye eneo hilo.
“Lengo letu ni kuhakikisha jamii ya eneo hii inanufaika kwenye sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, afya, maji na vikundi vya ujasiriamali,” alisema Toima.
Hivi karibuni wananchi wa kata ya Komolo waliliomba shirika la ECLAT Foundation kuwajengea madarasa matatu ya shule hiyo ili wanafunzi wapate eneo la kusomea