Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiongea na wananchi wa Mbingu, Kata ya Igima, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro Septemba 15.2019
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi wa Kata ya Mchombe, wilayani Kilombero, kwenye mkutano wa hadhara, Septemba 15.2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Kata ya Mrimba, wilayani Kilombero, kwenye mkutano wa hadhara, Septemba 15.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
……………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema changamoto ya barabara ya kutoka Ifakara hadi Mlimba iliyokuwa inawakabili wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu imepatiwa ufumbuzi baada ya Serikali kupanga kuijenga kwa kiwango cha lami.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha miundombinu ya barabara nchini ikiwemo barabara ya kutoka Ifakara hadi Mlimba yenye urefu wa km. 126.5.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumapili, Septemba 15, 2019) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Matangini, Mlimba wilayani Kilombero.
“Serikali imedhamiria kuimarisha barabara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Ifakara-Mlimba kwa kiwango cha lami lengo likiwa ni kurahisisha usafiri pamoja na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.”
Alisema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya wananchi na kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, hivyo aliwataka wananchi hao waendelee kuiamini Serikali yao.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Jackson Mpankuli ahakikishe amepeleka walimu katika shule ya msingi Matangini na Mwangazaambazo zinakabiliwa na upungufu wa walimu.
Waziri Mkuu alisema hadi Sepetemba 30 mwaka huu kiongozi huyo awe ameshawahashimia walimu katika shule husika. Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Suzan Kiwanga kulalamikia upungufu wa walimu hao.
Mbunge huyo alisema katika jimbo kuna tatizo kubwa la upungufu wa walimu hali inayosababisha baadhi ya wazazi kukodi walimu kwa ajili ya kuwafundisha watoto wao, hivyo Waziri Mkuu aliagiza walimu wahamishiwe katika shule ndani ya wiki mbili.
Akizungumza na wananchi katika eneo la Mchombe alipokuwa njiani kuelekea Mlimba, Waziri Mkuu aliwataka wazazi, walezi na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro kuhakikisha wanadhibiti ongezeko la mimba kwa watoto wa shule.
“Lazima kuwalinda watoto wa kike ili wasipate mimba kwani watashindwa kuendelee na masomo, hivyo watashindwa kutimiza ndoto zao. Viongozi simamieni utekelezaji wa sheria kwa kuwachukulia hatua wote waliowapa mimba wanafunzi.”
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa jimbo la Kilombero, Lijualikali na Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga waliiomba Serikali iwasaidie ujenzi wa barabara za kutoka Ifakara hadi Mlimba na barabara ya Ifakara hadi Kidatu ambayo ujenzi wake unasuasua.
Pia Suzan alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu kwa barabara ya Ifakara-Mlimba na baadae kuwekwa lami kwa awamu na kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ikiahidi kitu inatekeleza
Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro ambapo anatarajiwa kutembelea Halmashauri za wilaya ya Ulanga na Malinyi kukagua miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kuzungumza na wananchi pamoja na watumishi.