NA MWAMVUA MWINYI
OFISA Utafiti Mkuu kiongozi kutoka Tume ya Sayansi na teknolojia ,Dkt Bakari Msangi amesema katika kuelekea kwenye uchumi wa kati ,sayansi na utafiti ina mchango mkubwa kufikia adhma na malengo hayo.
Ameeleza, kuelekea uchumi wa kati ,ikumbukwe kwamba uchumi wa viwanda unategemea zaidi viwanda vya malighafi za kilimo ,uvuvi na mifugo.
Akizungumza katika kiwanda cha kuchakata maziwa cha Tanga Fresh, wakati wa mafunzo ya vitendo kwa baadhi ya waandishi wa habari kanda ya Mashariki na watafiti, yaliyoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na teknolojia kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la maendeleo la Sweden (SIDA ),Msangi alisema sayansi na utafiti ndio nguzo kwa wawekezaji wenye viwanda kuwahakikisha uzalishaji wa malighafi wanazozitegemea.
“Inasaidia ni wapi tunapata malighafi ya kutosha,kwasababu haina maana sana kuanzisha uzalishaji mfano wa ngano ya chapati wakati ngano mnayozalisha ni kidogo”
” Ni lazima mtafiti atafute ngano inayozalisha kwa wingi kwa mwaka mzima ili kumsaidia mwekezaji huyo azalishe kwa tija”alifafanua Msangi.
Nae kaimu mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa mifugo Tanzania ofisi ya Kanda, Zabron Nziku aliwataka wafugaji kubadilika kwa kufuga kisasa na kitaalamu .
Alielezea, wafugaji wakiweza kupanda aina bora za malisho,kuweka mabanda na kutumia utaalamu ya upandaji miche ya majani bora kwa ng’ombe kutoka katika taasisi hiyo basi wataongeza tija katika maziwa .
Awali meneja wa vyanzo vya maziwa Tanga Fresh, Nadomana Nyanga alibainisha ,kwa kushirikiana na Taasisi ya mifugo ya TALIRI wapo katika program ya kuangalia namna ya kuweza kuwalipa wafugaji kwa wanaozalisha kwa ubora.
“Zimbambwe wanafanya hivi, hivyo kwa Tanzania tukianza italeta maendeleo chanya kwa mfugaji ili afanye biashara ambayo ni endelevu”
Nadomana alisema kwasasa wanasindika lita 120,000 lakini wanazalisha lita 30,000 hadi 50,000 za maziwa kwa siku,kiwango kisichokidhi matakwa yao kutokana na uwezo wa wafugaji kupeleka maziwa kuwa mdogo.
Alifafanua kwamba, tukielekea katika uchumi wa kati inakadiriwa kila mtanzania hunywa maziwa lita 47 kwa mwaka na kutegemewa kufikia lita 100 kwa kipindi hicho kama ilivyo nchi ya Kenya.
Baadhi ya wafugaji Muheza ,Tanga akiwemo Sidori Charles alisema ,wana changamoto ya uhifadhi wa chakula cha kiangazi kwa ng’ombe ila kwa kupata elimu ameelewa ufugaji ng’ombe ni sayansi.