Mkurgenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Bw.Jimson Mhagama akiwasilisha ombi la Kampuni ya MDC ya uwekezaji wa vizimba vya samaki na maeneo ya kulima korosho,kakao na kahawa katika kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Kepten John Komba wilayani Nyasa.(picha na Ofisi ya Mkurugenzi Nyasa)
…………………….
Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma, imeridhia ombi la eneo la Uwekezaji wa vizimba vya samak,i kutoka Kampuni ya Mwanza Delights Compony ili kupunguza umaskini na kutokomeza uvuvi haramu Wilayani hapa .
akiwasilisha taarifa hiyo wakati wa kikao cha baraza la Madiwani, cha Wilaya ya nyasa kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Kepteni John komba Mjini Mbamba-bay, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nyasa Bw.Jimson Mhagama aliwataka wajumbe kujadiliana kwa umakini na kutoa maoni yao.
Bw Mhagama alifafanua kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa ilipokea ombi la eneo la uwekezaji pamoja na ujumbe wa watendaji wakuu kutoka kampuni ya mwanza Delights compony, ikieleza lengo la kampuni hiyo kuja kuwekeza Nyasa, katika Ufugaji wa samaki kwa kutumia Vizimba, na maeneo yanayofaa kwa kilimo cha kakao,kahawa na korosho.walipata uwepo wa maeneo hayo kupitia maonesho ya viwanda na biashara yaliyofanyika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Aliongeza kuwa, baada ya kutembelea maeneo kadhaa ya fukwe ambayo yaliainishwa na wataalam ujumbe kutoka mwanza Delights company ltd, uliridhishwa na eneo la fukwe ya puulu na kuona linafaa kwa ajili ya ufugaji kwa kutumia vizimba na maeneo ya Kijiji cha Lundo yanafaa kwa ajili ya Kilimo cha mazao ya biashara yaani Korosho,kahawa na kakao.
Aidha aliongeza kuwa ,mradi wa vizimba utawajumuisha na kuwashirikisha na kuwawezesha wavuvi katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Nyasa ili kufuga samaki. Utaratibu huu utachangia kupunguza umaskini na tatizo la uvuvi haramu kwa kiwango cha kikubwa katika Halmashauri yetu. Pia mpango wa mradi wa kilimo utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa jamii inayozunguka maeneo hayo, pamoja na kuongeza mapato ya ndani Katika Halmashauri ya Nyasa.
Baraza la madiwani kwa pamoja walikubaliana na taarifa hii na waliridhia kwa pamoja kupitia kwa Mwenyekiti wa Halmashauri Alto Komba ambaye ni mwenyekiti wa kikao na kuwaomba wawekezaji wengine kuja kuwekeza nyasa kwa kuwa kuna sehemu nyingi za uwekezaji.
“Napenda kuchukua Fursa hii kuwakaribisha sana wawekezaji katika Wilaya yetu ya nyasa kwa kuwa kuna Fursa nyingi za uwekezaji kwenye kilimo,ufugaji wa samaki wanyama,vivutio vya utalii vingi sana ambavyo viko nyasa” alisema komba.
Kampuni ya MDC imejipanga kimkakati kutekeleza mradi huu kwani imeshakamilisha taratibu zingine zinazotakiwa katika utekelezaji wa Mradi ,hivyo waliomba kibali cha kutumia maeneo haya kwa ajili ya uwekezaji na utekelezaji wa miradi hii na wapo tayari kulipa fidia na wanaendelea na utafiti wa maeneo mengine hasa ya fukwe za njia ya kusini kwa Kata ya ( Kilosa,Mtipwili na Chiwanda)