Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe (Katikati Mwenye suti Nyeusi) akikaribishwa na vijana wa
kimasai kwa wimbo maalum alipowasili kwa ajili ya kufunga serehe za kimila leo Jijini Arusha.
Mwenyekiti wa Viongozi wa Ukoo wa Wamasai Bw. Isack Lekisongo
akiongea jambo wakati wa ufungaji wa sherehe za kimila zilizofanywa na kabila hilo leo Jijini Arusha.
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe akiongea na Wazee wa Kimasai wakati wa kufunga sherehe za kimila za kabila hilo leo Jijini Arusha.
Baadhi ya Viongozi na Wazee wa Kimila wa kabila la Wamasai
wakifuatilia shughuli mbalimbali zilizokuwa zikifanywa wakati wa kufunga sherehe za kimila za kabila hilo leo Jijini Arusha.
Vijana wa kimasai wakicheza ngoma za kiutamaduni ikiwa ni ishara
ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na
Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (Hayupo katika picha) katika shughuli za kufunga sherehe za kimila leo Jijini Arusha.
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa
Serikali na Wazee wa kimila wa kabila la Wamasai katika shughuli ya kufunga sherehe za kimila leo Jijini Arusha.
(Picha na Lorietha Laurence-WHUSM,Arusha).
********************************
Na Lorietha Laurence-WHUSM,Arusha
Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe
awapongeza wazee na viongozi wa kimila wa kabila la kimasai kwa kuendeleza na kuhifadhi mila na desturi.
Hayo ameyasema leo Ngaramtoni, Jijini Arusha wakati wa kufunga
mafunzo ya kimila kwa vijana wa kimasai na kueleza kuwa mafunzo hayo
ni muhimu katika kumjenga kijana kuwa mtu mwenye maadili na kuheshimika kwa jamii yake.
“Mafunzo haya mliyoyapata kutoka kwa viongozi wenu na Wazee wa
kimila yanawajenga kuwa rai wema na wenye maadili katika kujenga taifa letu ” Dkt. Mwakyembe
Aidha aliongeza kwa kueleza kuwa Wizara inaunga mkono juhudi
zinazofanywa na Wazee wa Kimasai kwa kuhakikisha mila na desturi ya
mtanzania inatunzwa na kuendelezwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Pia Dkt. Mwakyembe ameahidi kushirikiana kwa karibu na Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi katika
kuhakikisha maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za mila yanahifadhiwa vizuri bila kuingiliwa na watu.
Vilevile aliwapongeza viongozi wa Jeshi la Tanzania kwa kuruhusu
maeneo ya kijeshi ambayo ni ya kihistoria kuendelea kutumika ajili ya
masuala ya kimila na kuzitaka taasi nyingine ambazo zina maeneo hayo kuiga mfano huo .
Naye Mwenyekiti wa Viongozi wa Ukoo wa Wamasai Bw. Isack Lekisongo
ameiomba serikali kulinda, kuhifadhi na kuendeleza mila na desturi za
jamii mbalimbali za kitanzania ili kupunguza madhara yanayoletwa na utandawazi.
“Ni muhimu kwa serikali yetu kutilia mkazo suala la kuhifadhi na
kuendeleza mila za jamii mbalimbali zilizopo nchini ili kuwa na taifa
lenye kuheshimu na kudumisha tamaduni zake” Bw. Isack Lekisongo
Anazidi kueleza kuwa kupitia mafunzo hayo yanayotolewa kwa vijana
yanawasaidia kujitambua,kuheshimu wakubwa na wadogo pamoja na
kuachana na tabia zisizofaa ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya.
Shughuli hizo za kimila za kimasai zilifunguliwa tarehe 6 Julai 2019 kwa
vijana kutoka katika sehemu mbalimbali za Tanzania pamoja na nchi
jirani ya Kenya ambao walipewa mafunzo kwa muda wa siku 100 na
kuhitimishwa tarehe 15 Septemba 2019 huku Dkt. Mwakyembe Waziri
mwenye dhamana ya utamaduni akiwa ndiye mgeni rasmi.