Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
akifuatilia majadiliano katika Kongamano la ‘Siku ya Mto Mara’ linaloendelea Mugumu – Sengereti Mkoani Mara. Kongamano hilo linaongozwa na kauli mbiu isemayo Nitunze Nikutunze. Wengine katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima.
*****************************
Na Ibrahim Mdee, Mara.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima
mwishoni mwa wiki ameshiriki katika kongamano la mto Mara linalofanyika Mugumu Wilaya ya Serengeti.
Katika kongamano hilo Naibu Waziri Sima amekuwa Mwenyekiti katika mjadala uliohusu Utunzaji wa Mazingira na uhifadhi wa Ikolojia ya Mto Mara.
Naibu Waziri Sima amesema kuwa maadhimisho ya siku ya mto Mara ni jitihada za
viongozi wakuu wa nchi zetu mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Kenya kwa upande mwingine. “Ushirikiano wao ndio unaendeleza jitihada hizi za kuutunza mto huu muhimu” Sima alisisitiza.
Akizungumzia Malengo ya Siku ya Mto Mara Sima ameainisha kuwa ni kukutanisha
jamii za pande zote mbili za nchi, kuona na kutambua faida za uhifadhi wa mto Mara kwa kuzingatia wajibu wa kila mmoja, kwa kuwa imebainika Bonde hilo linakabiliwa na Changamoto kubwa za uharibifu wa mazingira zitokanazo na shughuli zisizoendelevu za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na uvuvi.
“Hivyo kwa kutambua Changamoto hizi ni lazima wananchi wapewe taarifa sahihi za uharibifu na wajibu wao katika uhifadhi wa mto mara, Uharibifu ukiendelea kuna hatari ya Kupoteza ikolojia nzima ya mto Mara, hivyo mto utakauka na kusababisha atharikubwa kwa jamii na wanyama katika hifadhi yetu ya Serengeti na Maasai Mara huko Kenya” Sima alifafanua.
Imebanika kwamba takribani watu milioni 1.3 wanategemea uwepo wa bonde la Mto Mara katika shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji. Hata hivyo kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu ambalo halina uwiano na matumizi ya bonde la mto Mara, hivyo kuongezeka kwa idadi ya watu kumeongeza uharibifu wa uoto wa asili.
Aidha, imeelezwa kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na gugu vamizi
ambalo linaathiri mimea ya asili hasa majani ambayo yanasaidia kuhifadhi uoto wa asili ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanachangia katika uharibifu wa Mazingira katika bonde la mto Mara.
Katika majadiliano hayo imedhihirika kuwa uharibifu mkubwa Uko uwanda wa juu
(upstream) maeneo ya Kenya na uwanda wa chini (downstream) na Ili kukabiliana na hali hiyo imependekezwa kuanzishwa kwa chanzo cha kudumu cha Fedha kwa ajili ya kushughulikia uhifadhi wa bonde la Mara.
Pia, watafiti wa mazingira ikiwemo taasisi za elimu kuendelea kufanya tafiti zinazoweza kuibua njia sahihi za uhifadhi wa bonde la mara ikiwa ni pamoja na ushirikishwaji wa jamii inayoishi kandokando ya mto Mara.
Kongamano hilo limeenda sambamba na uwasilishaji wa mada zinazotilia mkazo
umuhimu wa uhifadhi wa bonde la Mto Mara, na kuongozwa na kauli mbiu isemayo “Nitunze Nikutunze”