Waziri wa Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack
Kamwelwe(kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Bandari Tanzaznia (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko (kulia)
kuhusu kutua kwa Meli kubwa ya mizigo ya MV Grand Duke kwenye gati
jipya namba 0 katika Bandari ya Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA)wakiongoza baadhi ya magari kutoka kawenye meli kubwa ya mizigo
ya magari MV Grand Duke baada ya kutua hapo jana kwenye gati jipya
namba 0 ya Bandari ya Dar es Salaam.
Gari likitoka kwenye meli kubwa ya mizigo ya magari MV Grand
Duke baada ya kutua hapo jana kwenye gati jipya namba 0 ya Bandari ya
Dar es Salaam.
Meli kubwa ya mizigo ya magari MV Grand Duke ikiwa katika
bandari ya Dar es Salaam mara baada ya kutua hapo jana kwenye gati
jipya namba 0 ya Bandari hiyo ambalo ukarabati wake unaelekea mwisho.
************************************
Na Paschal Dotto-MAELEZO
15-09-2019.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe
amezikaribisha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa
Afrika (SADC) kutumia bandari ya Dar es Salaam mara baada ya ukarabati wake
hasa gati nambo sufuri kuanza kupokea mizigo.
Akizungmza Jijini Dar es Salaam alipotembelea kuona meli kubwa ya Mizigo ya
Magari ya kampuni ya Meli ya Mv Grand Duke iliyotua bandarini hapo jana, Waziri
Kamwelwe alifurahishwa kuona meli hiyo kubwa nyenye urefu wa mita 200 na
uwezo wa kubeba magari 6,000 ambapo imetua ikiwa na magari 1,347
imedhihirisha uwezo wa bandari hiyo kwamba iko tayari kupokea mizigo mikubwa.
“Tuko hapa kuwahabarisha Watanzania, na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), kwamba ukarabati wa Bandari ya Dar es
Salaam unaenda vizuri ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa gati namba moja, mbili
na hili gati namba sifuri liko mwishoni na limeanza kupokea meli kubwa za Mizigo
kama mnavyoona hapo, hiyo ni meli ya mizigo ya magari yenye uwezo mkubwa
sana”, Waziri Kamwelwe.
Malengo ya Serikali ni kufanya ukarabati wamagati nane ambapo mpaka sasa gati
namba moja na gati namba mbili yako kwenye matumizi mara baada ya kukamilika
na sasa meli zinaendelea kutoa huduma kama kawaida, gati namba sifuri ambalo ni maalum kwa meli za mizigo ya magari linaendelea na ukarabati lakini asilimia
kubwa liko vizuri.
Waziri Kamwelwe alisema kuwa mara baada ya gati hilo kukamilika Tanzania
itakuwa na uwezo mkubwa wa kupokea mizigo ya magari laki 6 kwa mwaka, lakini
pia bandari hiyo inabeba tani milioni 17 kwa mwaka huku malengo ya Serikali ikiwa ni kufikia tani milioni 25 ifikapo mwaka 2021.
“Malengo yetu ni kufikia tani milioni 25 kwa mwaka tofauti na tani za sasa milioni
17, kwa hiyo Nchi Wanachama wa SADC, bandari hii sasa inafanya kazi vizuri, kwa
hiyo majirani zetu kutoka SADC, DRC, Malawi, Zambia na nchi zingine za ukanda
huu wa Kusini mwa Afrika wanakaribishwa sana kutumia bandari ya Dar es Salaam” Alisisitiza Waziri Kamwelwe.
Waziri Kamwelwe alisema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na
wafanyabiashara kutoka Nchi Wananchama wa SADC ili maeneo ambayo yana
changamoto ziweze kutatuliwa haraka.
“Serikali imewekeza fedha nyingi katika ukarabati huo, kwa hiyo itahakikisha kuwa inaipa bandari hii mizigo ya kutosha na hasa kutoka kwa Nchi Wanachama wa SADC, ili kuwawezesha kupata huduma rahisi za usafirishaji” alisema Kamwelwe.
kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, Mhandisi Deusdedit
Kakoko, alisema kuwa gati jipya namba sufuri limeanza kufanya kazi kwa kupokea
meli kubwa ya Mv Grand Duke ambayo imetua jana na mzigo wa magari 1347.
“ Hili gati ni Jipya ni kati ya magati nane ambayo yanajengwa, lenyewe
limejengwa kwa zege kama mnavyoona, lina uwezo wa kubeba magari 10,000 kwa wakati mmoja kutoka uwezo wa kubeba magari 2,500 ambao tulikuwa nao hapo mwanzo, lakini pia lina urefu wa mita 320 kwa hiyo ni gati kubwa na hii meli ina urafu wa mita 200 kwa hiyo kuna mita 120 zimebakia kwenye gati hili”, Alisema Mhandisi Kakoko.
Gati hilo ambalo ni la kisasa Zaidi litakuwa na taa ambazo zitawezesha kufanyika
kazi usiku na mchana hapo bandarini, na makabidhiano ya gati hilo yatafanyika
kesho ambapo Mkandarasi ataikabidhi Mamlaka ya Bandari (TPA).
Aidha, Mhandisi Kakoko alisema kuwa meli ya Abiria ziwa nyasa imeingia kwenye
majaribio ya mwezi mmoja ambapo mwezi ujao inatarajiwa kukabidhiwa kwa
Mamlaka hiyo ili kuanza kuhudumia wananchi wa maeneo hayo.