Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao wilayani humo.
Baadhi ya watumishi wa umma wilayani Sengerema wakimsikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao wilayani humo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (katikati) akisikiliza maswali ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao wilayani humo.
Mkurugezi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Bw. Ibrahimu Mahumi akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiutumishi kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Katibu Mkuu Utumishi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma wilayani humo.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akisoma moja ya nyaraka za aliyekuwa mtumishi wa umma, Bw. Boniventura Bwire ambaye alifanya udanganyifu ili kujipatia fedha za Serikali kinyume na taratibu za kiutumishi
……………….
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Bw. Boniface M. Magesa kwa kushirikiana na Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) kumtafuta popote alipo aliyekuwa mtumishi wa umma Bw. Boniventura Bwire na kumfikisha katika vyombo vya dola kwa kosa la kujipatia fedha za Serikali kwa udanganyifu katika kipindi cha miaka nane licha ya kufukuzwa kazi mwaka 2011.
Dkt. Ndumbaro ametoa maelekezo hayo wilayani Sengerema, wakati wa kikao kazi chake na watumishi wa halmashauri hiyo chenye lengo la kusikiliza changamoto za kiutumishi zinazowakabili na kuzitatua, ikiwa ni pamoja na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Dkt. Ndumbaro ameeleza kuwa, Bw. Bwire alikuwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mpaka mwaka 2011 kabla ya kufukuzwa kazi mwaka 2012 na mwajiri wake baada ya kugundulika kuwa na Stashahada ya Juu ya Uhasibu ya kughushi (advanced Diploma) ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).
Dkt. Ndumbaro amefafanua kuwa, mtumishi huyo alighushi barua za Katibu Mkuu TAMISEMI na kufanikiwa kuhamia katika Halmashauri za Wilaya ya Ukerewe, Bariadi na hatimaye Sengerema.
“Kwa miaka nane Bw. Bwire amekuwa akifanya kazi Serikalini akiwa sio mtumishi wa umma halali baada ya kufukuzwa kazi na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara, na katika halmashauri zote alizohamia amekuwa akijitambulisha kama Afisa Mapato na kufanya kazi hiyo na hatimaye kujilipa, hivyo kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu”, amesema Dkt. Ndumbaro.
Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa, baada ya mtumishi huyo kuhamia Sengerema, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kutokana na umakini wake aliweza kubaini kuwa, mtumishi huyo anatumia cheti cha kidato cha nne ambacho si chake hivyo akamfukuza kazi.
Dkt. Ndumbaro amesema, Mtumishi huyo baada ya kufukuzwa kazi aliwasilisha rufaa yake kimakosa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) badala ya Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ndio mamlaka yake ya rufaa.
Sanjali na hayo, Dkt. Ndumbaro amesema, atawasiliana na Katibu Mkuu TAMISEMI ili afanye uchunguzi na kumtaka kumchukulia hatua stahiki mtumishi wa TAMISEMI atakayebainika kumsaidia Bw. Bwire kufanikiza azma yake ya kuiibia Serikali.
Dkt. Ndumaro amehitimisha kwamba, mambo yote aliyoyafanya Bw. Boniventura Bwire tangia mwaka 2011 hadi sasa ni batili kwani si mtumishi wa umma halali baada ya kufukuzwa kazi, na hakuwahi kukata rufaa kwenye mamlaka stahiki, hivyo kutokana na makosa yake kuwa ni ya jinai ameelekeza suala la mtumishi huyo liwasilishwe Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa uchunguzi na kulifikisha mahakamani haraka iwezekanavyo ili Sheria ichukue mkondo wake.