Wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Nsemulwa wakiwa wamesongamana darasani.
Mwalimu akiwa na wanafunzi nje ya darasa akiwafundisha kuandika chini.
******************************
Changamoto ya wingi wa wanafunzi; uhaba wa vyumba vya madarasa na ukosefu wa zana za kufundishia na kujifunzia kwa madarasa ya awali na darasa la kwanza katika baadhi ya shule za msingi za manispaa ya mpanda mkoani katavi zinapelekea wanafunzi kutolewa nje ya darasa kujifunza kuandika katika mchanga; hali ambayo licha ya kusababisha usumbufu kwa walimu pia inawaacha wanafunzi wakiwa wamechafuka
Wakizungumzia hali hiyo walimu wa madarasa ya awali; wametoa wito kwa wadau kujenga vyumba vya kutosha vya madarasa
Bi. Agatha Mgoloka ni Mwalimu wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Nsemulwa amesema kutokana na chumba kimoja kutumiwa na zaidi ya darasa moja wanashindwa kubandika picha za kufundishia watoto wadogo ukutani
Aliongeza kuwa hali hiyo inachangia kuwa na madarasa bubu
“Chumba hiki asubuhi wanaingia darasa la kwanza lakini mchana wanakitumia darasa la tano kwa hiyo ukibandika picha za wadogo wakija wakubwa wanazing’oa” alisema
Aidha upungufu wa madarasa unachangia kuwepo kwa msongamano mkubwa wa watoto na hivyo kushindwa kutumia madawati kwa wanafunzi wote
Ukiweka madawati kote hawatoshi watoto ni wengi mpaka mbele ya darasa” aliongeza mwalimu Mgoloka
Naye mwalimu wa darasa la awali katika shule hiyo Yusta Machilima alisema kutokana na kutokuwepo kwa vibao vya kujifunza kuandika kwa wanafunzi huwa anawatoa nje na kuwafundisha kuumba herufi katika mchanga
“Wanajifunza na wanaandika vizuri ila wanachafuka sana, kiasi kwamba mpaka wakati wa kutoka shule mtoto anakuwa mchafu sana” alisema mwalimu Machilima
Kwa upande wake Mratibu Kiongozi wa Mpango wa Kuinua Elimu Nchini (Equip-T) Bwana Laurent Mpuya amesema Mpango umekuwa ukitoa fedha kwa ajili ya umaliziaji wa vyumba vya madarasa
Alieleza kuwa fedha hizo zinapelekwa katika halmashauri husika na kisha halmashauri inagawa katika shule zao
“Mfano hapo Nsemulwa wamepokea kiasi cha shilingi milioni kumi kumalizia jingo la vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu” alisema Mpuya
Naye Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Mpanda Godfrey Kalulu amekiri kutokuwepo kwa madarasa yanaoongea katika shule nyingi za manispaa hiyo kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa
Aidha ametoa wito kwa walimu kutumia mazingira waliyonayo kutengeneza vifaa vya kujifunzia hata kwa kuwashirikisha wanafunzi wao pia
Shule ya msingi Nsemulwa ina zaidi ya wanafunzi elfu tatu na ina vyumba saba tu vya madarasa hali inayopelekea wanafunzi kujifunza kwa awamu mbili