JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LINAWASHIKILIA WATUHUMIWA NANE KWA TUHUMA ZA KUJERUHI.
Tarehe 11.09.2018 saa 10:00 asubuhi huko katika Kijiji cha Msesule, Kata ya Mapogoro, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali kundi dogo la wakulima “scheme” ya umwagiliaji ya Mahalala wakiwa shambani kwao wanasafisha mfereji wa umwagiliaji maji walivamiwa na wananchi wa Kijiji cha Msesule wakiongozwa na watu wawili ambao majina yao tunayahifadhi kwa sababu za kiupelelezi, miongoni mwa watuhumiwa hao ni Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Msesule ambaye anaendelea kutafutwa mara baada ya kukimbilia kusikojulikana. Inadaiwa kuwa, watuhumiwa hao wakiwa na silaha za kienyeji / jadi zikiwemo mapanga, mikuki na mishale waliwajeruhi watu kumi na moja [11] maeneo mbalimbali ya miili yao ambapo nane [08] kati yao walitibiwa na kuruhusiwa na wahanga watatu bado wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali.
Aidha baada ya kutekeleza uhalifu huo watuhumiwa hao pia walifanya uharibifu wa Pikipiki tano ambazo ni mali za wanakijiji cha Mahalala.
Kufutia tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako mkali na kufanikiwa kukamata watuhumiwa nane [08] ambao bado wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo ambao ni:-
- DENIS SEGELE [36] Mkazi wa Ubaruku
- ANNOLD KIBODI [15] Mkazi wa Msesule
- AMOSI KITA [56] Mkazi wa Mabadaga.
- KAPILIPILI SICHURA [35] Mkazi wa Ubaruku.
- KASUKA BULHAMA [56] Mkazi wa Msesule
- EDWARD MBANGALA [37] Mkazi wa Makondeko na
- NEBATI TULYANJE [30] Mkazi wa Ubaruku.
- JUMANNE MASHAKA [52] Mkazi wa Msesule.
Chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa ardhi shamba yenye ukubwa wa ekari 300 baina ya wanakijiji cha Msesule na wanakikundi cha umwagiliaji wa Kijiji cha Mahalala ambapo shauri lao lililokuwa baraza la ardhi na nyumba Jijini Mbeya namba 107/2018 ambalo lilimalizika kwa kikundi cha umwagiliaji cha Kijiji cha Mahalala kushinda lakini Kijiji cha Msesule hawakukubaliana na maamuzi hayo hivyo walikata rufaa Mahakama Kuu Mbeya ambapo bado maamuzi hayajatolewa.
Baada ya Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Mbarali kuona taharuki hiyo yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, aliamua eneo hilo lisifanyiwe shughuli yoyote ya kilimo hadi maamuzi ya Mahakama Kuu Mbeya yatakapotolewa, jambo ambalo lilipuuzwa na pande zote mbili hali iliyosababisha kutokea kwa mapigano hayo yenye viashiria vya uvunjifu wa amani ambapo madhara yake ni majeruhi ya watu nane na uharibifu wa Pikipiki tano ambazo thamani yake bado kufahamika.
WITO:
Natoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya na Tanzania kwa ujumla hususani maeneo yenye migogoro ya ardhi kama vile Mbarali, Rungwe, Kyela na popote pale kuacha mara moja vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na wafuate sheria, kanuni na taratibu za nchi katika kutatua migogoro na kero mbalimbali zilizopo katika maeneo yao.
Aidha nawataka wananchi wote kuheshimu maelekezo yanayotolewa na mamlaka zilizopo na wajielekeze kutii sheria bila shuruti kwani Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya halitafumbia macho wala kusita kumchukulia hatua za kisheria yeyote atakayekiuka sheria.
JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA LINAWASHIKILIA WATUHUMIWA WAWILI KWA TUHUMA ZA WIZI.
Tarehe 11.09.2919 saa 12:09 mchana huko maeneo na Kata ya Uyole, Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limemkamata YUSUPH HUSEIN [20] dereva bajaji, mkazi wa ilemi akiwa na bajaji moja nyeusi aina ya TVS King yenye namba za usajili MC.341 BZT, namba ya sumatra 2597 ikiwa haina matairi yote matatu, kioo cha mbele ,block engine pamoja cylinder head.
Mtuhumiwa alipohojiwa alikiri kuiba bajaji hiyo maeneo ya Kabwe akiwa na wenzake na kupelekea kukamatwa kwa 1. FRANCIS SIMON [31] fundi bajaji na mkazi wa Uyole akiwa na vifaa mbalimbali vya bajaji ambavyo ni:-
- Mapaja mawili ya bajaji yenye drum zake,
- Tairi mbili zikiwa na rim zake,
- Starter moja pamoja na tanganyika jeck vifaa vyote vilichomolewa kwenye bajaji.
Wengine ni:- 1. ANOLD VALELIAN [24] Mkazi wa Sae. 2. DENIS ADE [28] Mkazi wa Airport ya Zamani na 3. KHALFAN SAID [19] Mkazi wa Airport ya Zamani.
Juhudi za kuwatafuta watuhumiwa wengine waliohusika katika wizi huo na mtandao wote unaojihusisha na wizi wa vyombo vya moto hapa Mbeya na mikoa jirani zinaendelea pamoja na kumpata mmliki halali wa bajaji hiyo.
WITO:
Natoa wito kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya wizi wa Pikipiki na Bajaji kuacha mara moja kwani uovu una malipo yake na Mbeya si salama kabisa kwa wahalifu wa aina yoyote ile. Pia wananchi wote wawe tayari kutoa ushirikiano kuvibaini vikundi mbalimbali vya kihalifu kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili liweze kuvishughulikia kwa mujibu wa sheria, hivyo kama wewe ni mhalifu uliyebahatika kujipenyeza na kuingia Mbeya kibahatibahati subiri “Mtiti” wake uko kisogoni mwako.
Aidha Operesheni nyingine za kuzuia na kupambana na uhalifu na wahalifu sambamba za zile za kudhibiti ajali za barabarani zimeshika kasi ili kuhakikisha Mkoa wetu unaendelea kuwa salama.