Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdini Babu akizindua upandaji miti pembezoni mwa mto Mara ilikuhakikisha wanalinda bonde la mto Mara.
*****************************
Jumla ya Miche 4,000 imependwa kando kando ya mto Mara katika kijiji cha Nyansurura wilayani Serengeti mkoani Mara ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Mara yanayofanyika wilayani Serengeti.
Akizungumza katika zoezi la pili la upandaji wa miti hiyo , Afisa Mazingira Wilaya us Serengeti, Victor Rutonesha alisema kuwa lengo la upandaji miti hiyo ni moja ya mikakati ya kuhakikisha kuwa mto huo ambao unakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira unahifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijazo.
Alisema kuwa ili kuhakikisha kuwa kiti hiyo iliyopandwa inakuwa endelevu tayari shamba hilo limekabidhiwa kwa uongozi wa serikali ya kijiji hicho ambao utakuwa na wajibu wa kutunza na kuhakikisha kuwa miti hiyo inakuwa huku halmashuri yake ikisismamia kwa ukaribu maendeleo ya shamba hilo.
Aidha Aliongeza kuwa tayari uongozi wa wilaya pia imekabidhi majembe 10 kwa klabu ya anatunza mazingira kati na shule ya sekondari Nyansurura kama njia mojwapo ya kuwawezesha wanafunzi hao kushiriki katika utunzaji wa shamba hilo.
Akiongea wakati wa upandaji wa miti hiyo, Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu alisema kuwa juhudi za makusudi zinahitajika ili kuhakikisha kuwa mto huo unaendelea kuwepo.
Alisema kuwa uwepo wa shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya mto huo ni miongoni mwa mambo yanayotishia uhai wa mto na kwamba umefika muda sheria za uhifadhi wa mazingira ikiwepo sheria inayozuia shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 katika mito mikubwa na mita 30 kwa mito midogo ziweze kutumika kutoa adhabu wa watakaobainika kufanya shughuli zao ndani ya hifadhi ya mto huo.
Babu aliagiza idara ya mazingira pamoja na mamlaka zingine zinazohusika kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwa wananchi ili waweze kuelewa juu ya sheria as uhifadhi w mazingira sambamba na umuhimu wa kuhifadhi mto huo muhimu kwa uchumi wa mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla.
Naye Afisa Tawala mkoa wa Mara msaidizi-Uchumi, Denis Nyakisinda alisema kuwa kuanzia sasa mifugo itkayokamatwa ndani ya ikolojia ya mto Mara itakamatwa na wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ni marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi ya mto lakini vitendo hivyo vimekuwa vinafanyika na kwamba umefika muda sasa sheria itaanza kuchukua mkondo wake huku akiwataka wananchi kuheshimu sheria hizo na kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira ya mto huo.