Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephani Chaula (katikati) akikagua miundomnbinu ya shule ya msingi Kimelok ambayo majengo yamejengwa na kukarabatiwa na shirika la ECLAT Foundation.
Wanafunzi na wazazi wa shule ya msingi Kimelok Kijiji cha Kimotorok Kata ya Loiborsiret Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakishuhudia makabidhiano ya miundombinu ya shule yao ambapo shirika la ECLAT Foundation lilitumia shilingi milioni 267 kujenga na kukarabati kisha kuikabidhi serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula watatu kushoto na viongozi wa shirika la ECLAT Foundation na Upendo Society wakipongezana baada ya uzinduzi wa shule ya msingi Kimelok Kijiji cha Kimotorok Kata ya Loiborsiret.
…………………..
Na.Joseph Lyimo,Simanjiro
SHIRIKA lisilo la kiserikali la ECLAT Foundation la Emboreet Wilayani Simanjiro, limetumia shilingi bilioni 6 katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii kwenye mikoa ya Manyara, Arusha, Mtwara na Kigoma.
Mwenyekiti wa ECLAT Foundation, Peter Toima aliyasema hayo wakati akiikabidhi serikali miundombinu ya shule ya msingi Kimelok ya kijiji cha Kimotorok kata ya Loiborsiret kwa mkuu wa wilaya ya Simanjiro Mhandisi Zephania Chaula.
Toima alikabidhi madarasa mapya na mengineyo yaliyokarabitiwa, nyumba mpya ya walimu na matundu 32 ya vyoo ambayo yamesababisha shule hiyo kuwa na muonekano mpya kwa gharama ya sh267 milioni.
Alisema katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi, ECLAT Foundation na shirika la Upendo la Ujerumani wamefanya hayo kuisaidia serikali kwenye mikoa tofauti nchini.
Alisema wamefanikisha miradi ya maendeleo ya elimu, maji na kuwezesha kiuchumi miradi ya vikundi, kwa kutumia fedha hizo kwa ushirikiano mkubwa wa shirika la Upendo la Ujerumani.
“Tumefanya haya kwenye maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilaya za Simanjiro Manyara, Monduli na Ngorongoro Arusha, Kakonko Kigoma na Tandahimba mkoani Mtwara,” alisema Toima.
Ofisa miradi wa ECLAT Foundation, Bakiri Angalia alisema kwa siku tatu mfululizo wataikabidhi serikali shule ya msingi Kimelok, shule ya msingi Nadoilchukini na Lengijape ya Lorkisalie ambazo wamejenga miundombinu au kukarabati.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula aliipongeza ECLAT Foundation kwa kufanikisha ujenzi wa miundombinu wa shule hiyo ya Kimelok ya Kimotorok.
“Tunawapongeza ECLAT Foundation na Upendo, sisi hatuna ubaguzi wa shirika lolote lile kwa hiyo mashirika mengine tunawakaribisha mlete maendeleo kwenye wilaya yetu ya Simanjiro,” alisema Chaula.
Mkazi wa kijiji cha Kimotorok, Namnyaki Isaya alisema hatua ya shirika la ECLAT Foundation ni kubwa katika kufanikisha mwanga wa elimu kwa wananchi wa wilaya ya Simanjiro.
Alisema mashirika kama hayo ndiyo yanatakiwa kuungwa mkono kwani yanajitoa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maendeleo kupitia miradi kama hiyo.