…………………………….
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesaini mkataba wa makubaliano wa miaka mitatu na serikali ya Ujerumani kwa ajili ya kuimarisha afya ya msingi nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainabu Chaula alisema kuwa wizara yake imesaini mkataba huo na serikali ya Ujerumani katika kuboresha sekta ya afya katika maeneo manne ambapo sekta hiyo itapata kiasi cha shilingi za kitanzania Bilioni 26.6.
” Kwa kweli niwashukuru sana wenzetu wa Serikali ya Shirikisho la Ujerumani kwa namna ambavyo wamekua bega kwa bega na sisi, zaidi niwapongeze na kuwashukuru ndugu zetu wa GIZ hawa wamekua wadau wakubwa wa Afya nchini.
” Tunawaahidi kuwapa ushirikiano na kusimamia kwa ukamilifu yale yote tuliyokubaliana kuyatekeleza, lengo letu sote ni kuona sekta hii ya afya inakua na inawanufaisha Watanzania ambao ndio haswa walioipa dhamana Serikali ya awamu ya tano kuwatumikia,” Amesema Dk Chaula.
Aidha amelipongeza Shirika hilo kwa kukubali kuwapatia fedha hizo kwa wakati mmoja ili iwe rahisi kuweza kutekeleza maazimio yote kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
” Ndugu zangu kazi ya Serikali ni kuwaletea wananchi wake Maendeleo na Rais wetu Dk John Magufuli ni mtu wa vitendo haswa, amedhamiria kuifanya Nchi yetu kuwa imara katika kila nyanja na afya ikiwemo, haya yote tunayoyafanya leo ni matokeo ya juhudi kubwa ambazo yeye kama Kiongozi wetu wa Nchi amekua nazo,” Amesema Dk Chaula.
Naye Mkurugenzi mkazi wa Shirika la Maendeleo GIZ, Dk Mike Falken amesema makubaliano waliyoyafikia na Wizara ya Afya ni matokeo ya utendaji kazi wa Serikali ya Tanzania katika kuwatumikia wananchi wake.
Aidha Dk.Falken amesema kuwa mkataba huo umejikita katika afya ya msingi hasa katika zahanati na vituo vya afya na utalenga maeneo matano ambayo ni Uboreshaji wa Taarifa, Mama na Mtoto, Bima, Uzazi wa Mpango na Utawala Bora.
” Sisi tunawaahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati yetu, sisi tunaridhishwa na kasi ya Rais Magufuli katika kuwatumikia Watanzania na ni wazi tunamuunga mkono kwa vitendo,” amesema Dk Falken.
Awali Shirika hilo lilikabidhi kwa Serikali kupitia Wizara ya Maji mradi wa Maji katika eneo la Nghong’onha jijini Dodoma ambao umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 331 na utahudumia wananchi takribani 12000.