Home Biashara ONGEZEKO LA IDADI YA WATU NCHINI NI FURSA KWA UKUAJI WA UCHUMI

ONGEZEKO LA IDADI YA WATU NCHINI NI FURSA KWA UKUAJI WA UCHUMI

0

Na. Josephine Majura na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

Serikali imeeleza kuwa ongezeko la idadi ya watu nchini ni fursa ya ukuaji wa uchumi kwa kuitumia kama nguvu kazi ya kuzalisha mali, soko la bidhaa na huduma.

Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Bunda Vijijini , Mhe. Boniface Getere, aliyetaka kujua faida ya ongezeko la idadi ya watu na mikakati ya Serikali ya kudhibiti ongezeko hilo.

Dkt. Kijaji alisema kuwa, Taifa la Tanzania bado lina rasilimali asili za kutosha kama ardhi ya kulima, bahari, maziwa, mito, mabonde, madini, misitu, jiografia ya usafiri pamoja na fursa za utalii ambazo zikitumiwa kikamilifu, uzalishaji mali utaongezeka na kupunguza umasikini badala ya kuogopa ongezeko la watu.

 “Si jambo baya kudhibiti ongezeko la idadi ya watu kama familia au Taifa limefikia kiwango cha mwisho cha kutumia rasilimali zake za asili pamoja mikakati mingine mbadala”, alieleza Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa, kwa sasa Serikali imejielekeza zaidi katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kufanya biashara ili kutumia kikamilifu nguvu kazi iliyopo nchini kukuza uchumi.

Dkt. Kijaji alisema utafiti wa idadi ya watu Duniani unaonesha idadi kubwa ya watu ni fursa iwapo kutakuwa na maboresho katika maisha ya watoto, elimu na uwezeshaji kwa wanawake na  kuimarisha uwekezaji katika afya ili kuwa na nguvu kazi bora na yenye tija.

Maeneo mengine ni kuimarisha uwekezaji katika elimu ya juu ili kuwa na nguvu kazi yenye elimu, ujuzi na ubunifu, kufanya mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kuharakisha ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa kazi kwa ajili ya nguvu kazi iliyopo na mageuzi ya sera ili  kuvutia wawekezaji wa kigeni na kuhakikisha uwajibikaji hasa katika rasilimali za umma.

Aidha alieleza kuwa  dhima ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 hadi 20220/ 2021 ni  kujenga uchumi wa viwanda ili kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.

Alisema Mpango huo wa pili umejikita zaidi katika uwekezaji wa kimkakati katika Sekta ya viwanda, kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kusambaza umeme mijini na vijijini, kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakati na kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kujenga Bwawa la kufua umeme katika mto rufiji.

Alibainisha kuwa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano unalenga kuimarisha huduma za jamii kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya maji, shule, hospitali vituo vya Afya vya umma, pamoja na kutekeleza kwa ufanisi sera ya Elimu bila malipo.

Dkt. Kijaji aliongeza kuwa, miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inalengo la kufungamanisha fursa za kiuchumi na ongezeko la idadi ya watu.

Matokeo chanya ya ongezeko la watu nchini yataonekana iwapo kila Mtanzania atashiriki kikamilifu katika uzalishaji mali na huduma za jamii kuanzia ngazi ya Kaya hadi Taifa.