Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa kongamano linalohusisha wadau mbalimbali wa masuala ya UKIMWI linaloendelea Jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia moja ya bidhaa zinazotengenezwa na kikundi cha wajasiriamali waliokua wanatumia madawa ya kulevya kabla ya ufunguzi wa kongamano la wadau mbalimbali wanaojihusisha na takwimu za ugonjwa wa UKIMWI linaloendelea jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile (wa tatu kulia) akijadiliana jambo na makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii Mhe. Juma Nkami (wa kwanza kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa NIMR prof. Yunus Mgaya na wengineo baada ya kumaliza ufunguzi wa kongamano la wadau mbalimbali wanaojihusisha na masuala ya tafiti za UKIMWI nchini linaloendelea jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akiwa katika picha ya pamoja na washiriki mbalimbali wanaohudhuria kongamano la wadau wanaohusika na masuala ya tafiti za ugonjwa wa UKIMWI linaloendelea jijini Arusha.
Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Juma Nkamia akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau mbalimbali wa masuala ya tafiti za ugonjwa wa UKIMWI linaloendelea Jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia moja ya bidhaa zinazotengenezwa na kikundi cha watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI wakati alipotembelea mabanda mbalimbali kabla hajafungua kongamano la wadau wa Masuala ya UKIMWI linaloendelea Jijini Arusha.
……………………………………………..
Na WAJMW-ARUSHA
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ametaka maboresho ya mifumo ya takwimu za tafiti mbalimbali zinazofanyika nchini.
Dkt. Ndugulile amesema hayo wakati akizindua kongamano linalohusisha wadau mbalimbali wa masuala ya UKIMWI ambao wanawasilisha tafiti na takwimu mbalimbali ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi nchini.
“Tunahitaji tuboreshe mifumo yetu ya takwimu ili tuwe na uwiano wa takwimu ambazo zinawasilishwa katika mkutano huu, hapa nimeona takwimu mbalimbali zimewasilishwa, ninaomba takwimu hizo ziwe za wote kwa sababu tuna wadau wengi wanaoshiriki katika mapambano haya dhidi ya Ugonjwa wa UKIMWI hivyo maelekezo yangu kuwe na mfumo mmoja wa takwimu ambao kila mmoja atakua anachangia takwimu zake na mfumo huo uwe wa mwisho utakaotoa takwimu za wote”. Amesema Dkt. Ndugulile.
Hata hivyo Dkt. Ndugulile amehamashisha makongamano kama hayo yafanyike mara kwa mara ili kuwawezesha wanazuoni, watunga sera na walengwa kukaa pamoja ili kujadiliana mambo mbalimbali ambayo yanahusuana na afua ambazo zinatekelezwa hapa nchini.
Kongamano hilo limeshirikisha taasisi za Serikali ambazo ni NIMR na TACAIDS pamoja na wadau mbalimbali wanaofanya tafiti kuhusiana na ugonjwa wa UKIMWI ambao wamekutana ili kuwasilisha takwimu za tafiti mbalimbali ambazo wanazifanyia kazi katika maeneo yao.