Menejimenti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na
Watumishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala na Serikali za Mitaa na Idara
maalum ya Zanznibar wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa Mhe. Selemani Jafo wakati akifungua kikao kazi
kilichofanyika katika Ofisi za OR-TAMISEMI Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Mhe. Selemani Jafo
akiongea na menejimenti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa na Watumishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala na
Serikali za Mitaa na Idara maalum ya Zanznibar wakati akifungua
kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi za OR-TAMISEMI Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Mhe. Selemani Jafo
wakati akiwa katika picha ya pamoja Watumishi kutoka Ofisi ya Rais
Tawala na Serikali za Mitaa na Idara maalum ya Zanznibar mara
baada ya kufungua kikao kazi kilichofanyika katika Ofisi za OR-
TAMISEMI Jijini Dodoma.
*********************************
Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI
Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema ili Mamlaka za Serikali za Mitaa ziweze kujiendesha lazima kuwepo na demokrasia ambapo ugatuaji wa madaraka ni muhimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa
Ameyasema hayo leo wakati akifungua Kikao kazi kati ya Menejimenti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Watumishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala na Serikali za Mitaa na Idara maalum ya Zanznibar kilichofanyika katika Ofisi za OR-TAMISEMI Jijini Dodoma.
Mhe. Jafo amesema katika kuhakikisha wananchi wanapata viongozi bora katika jamii Ofisi ya Rais TAMISEMI husimamia viongozi wa vijiji wasiopungua 12,000, viongozi wa Mitaa ambao wao wanapatikana katika Majiji, Manispaa na Halmashauri za Mijiambao ni zaidi ya 4000 na viongozi wa vitongoji zaidi ya elfu 64.
Amefafanua kuwa OR-TAMIEMI ni kiungo muhimu katika kusimamia utekelezaji wa sera mbalimbali zinazoandaliwa na Wizara zote nchini hivyo inaposhindwa kutimiza majukumu yake, kunakuwepo na ongezeko kubwa la Malalamiko kwa wananchi.
“Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ni kiungo muhimu katika Sekta zote ambapo isipotimiza wajibu wake kwa weledi haitatimiza lengo la Serikali la kuhakikisha uwepo wa maendeleo katika kila sekta nchini” Amefafanua Jafo.
Amesema kuwa OR-TAMISEMI ni watekelezaji wa Sera na miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara za Kisekta kwa kuwa ndio yenye Halmashauri ambazo hutoa huduma kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji na mtaa lengo likiwa ni kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Amezitaja Taasisi ambazo zipo chini ya OR-TAMISEMI kuwa ni elimu Kibaha ambayo inasimamia masuala ya elimu, Taasisi ya Mabasi ya Mwendokasi, Chuo cha Hombolo ambacho kinaendesha mafunzo kwa ajili ya kutengeneza watumishi watakaosimamia utendaji kazi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa
Mhe. Jafo amesema ugatuaji wa madaraka hufanyika pia katika Sekta ya Elimu ambapo kazi ya Wizara ya Elimu ni kutunga Sera na miongozo mbalimbali wakati OR-TAMISEMI kazi yake ni kusimamia miundombinu ya Elimu kuanzia ngazi ya Msingi hadi Sekondari lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa elimu nchini.
Hata hivyo amesema kwa upande wa Sekta ya Afya Serikali imeweza kufanya mabadiliko makubwa ambapo mpaka sasa Hospitali za Wilaya 67 zinajengwa na Vituo vya kutolea huduma 352 vimekarabatiwa na kujengwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Amewataka watumishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Serikali za Mitaa na Idara maalum kutoka Zanzibar kujifunza kazi zinazofanywa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tanzania Bara ili waweze kufanyia kazi yale ambayo watayapata katika kikao kazi hicho.
Wakati huohuo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Joseph Nyamhanga amewapongeza watumishi hao kwa kuamua kujifunza kuhusu ugatuaji wa madaraka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu katika majukumu ili kuleta mabadiliko katika jamii.
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala na Serikali za Mitaa na Idara Maalum Zanzibar Mhe. Shamata Khamisi amesema kuwa lengo la ujio wao ni kubadilishana uzoefu kwa kuwa Zanzibar imeanza kupeleka majukumu kwa wananchi ikiwa ni ugatuaji wa madaraka.
Amesema kuwa kwa upande wa Zanzibar utekelezaji wa Sera ya ugatuaji wa madaraka inatakribani miaka miwili ambapo yapo mafanikio ambayo yanaonekana hivyo ni wajibu wetu kuja kujifunza zaidi juu ya ugatuaji wa madaraka ili kuweza kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.