Na.Alex Sonna,Kongwa
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe Deo Ndejembi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani humo kuchunguza mapato yanayopatikana kwenye Hospitali ya Wilaya hiyo.
DC Ndejembi ametoa maagizo hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye Hospitali hiyo ya Wilaya na kukagua mapato ambayo yamekua yakipatikana hasa kwenye fedha za papo kwa papo.
Amesema ziara hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa za baadhi ya watumishi wa Hospitali hiyo kutokua waaminifu kwenye uandikishaji wa wagonjwa wale wanaolipa fedha za hapo kwa hapo.
” Nimefanya ziara hii kwenye Hospitali yetu ya Wilaya kuangalia fedha zile za papo kwa papo. Nilikua na ‘cashier’ hapo na tumekagua mapato na kugundua kumekua na ukusanyaji fedha wa kutiliwa mashaka.
” Kwa taarifa tulizonazo kuna baadhi ya watumishi huwa wanafanya ujanja pale mgonjwa anapokuja, kwa maana akija mgonjwa ambaye analipia yeye huchukua taarifa zake kana kwamba yupo kwenye makundi maalum yale ambayo hayakatwi tozo kama wazee, sasa nimeagiza mara moja Takukuru wafanye uchunguzi kubaini hii hali.
” Mfano hapa tumeangalia mapato ya siku kwa siku. Kuna siku mapato yanafika laki saba, siku nyingine tukaona ipo 37,000 lakini leo hapa tumekuta 350,000. Ni jambo ambalo tumelitia mashaka,” amesema DC Ndejembi.
Aidha ameitaka Takukuru kupitia taarifa zote za kibenki za Hospitali hiyo ili kuangalia pia kiasi ambacho kinahifadhiwa kwenye akaunti ni sahihi.