Home Siasa NAIBU KATIBU MKUU WAZAZI ATOA SOMO UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

NAIBU KATIBU MKUU WAZAZI ATOA SOMO UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

0
******************
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi, Kija Magoma amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilipoteza baadhi ya vijiji, vitongoji,mitaa, kata na majimbo kwa fitna na uzembe wa wanachama wake na kuwataka wasirudie makosa kwenye chaguzi zijazo.

Pia kimeonya wana CCM wanaojipitisha kwenye majimbo na kata  wakifanya kampeni za siri na kuanza kuchafuana na kuagiza majina yao yaorodheshwe ili washughulikie kwa sababu wanakichafua Chama.

Magoma alitoa kauli hiyo jana jijini Mwanza, kwenye kongamano la elimu, maadili,afya,mazingira, siasa na uchumi lililoandaliwa na Wazazi Wilaya ya Nyamagana, kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.

Alisema mwaka 2014 na 2015 CCM ilishindwa kwenye baadhi ya maeneo kwa sababu ya fitna, majungu, kusemana vibaya (kuchafuana)  na uzembe wa wanachama wake pindi uchaguzi unapokaribia, hivyo uchaguzi wa mwaka huu wasirudie makosa hayo.

“Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu ni wa kuonyesha dira ya 2020.Chama kwanza, mtu baadaye na tuache majungu, fitna,kuchafuana na kutukanana, ikitokea hivyo hao tunaowachafua tukawapitisha itakuwa fimbo ya kutuadhibu itakayotumiwa na wapinzani,”alisema Magoma.

Alisema wapo wana CCM kote nchini wanajipitisha kabla ya wakati wakifanya kampeni za siri ili wapitishwe kugombea uongozi na kuonya muda huo haujafika na wanaofanya hivyo wasidhani wako salama,wataanza kuchukuliwa hatua wilayani  kwa sababu wanaichafua CCM.

“Angalizo, serikali ya Rais John Magufuli si ya mchezo, wanaofanya kampeni za ubunge na udiwani kabla ya wakati wanafahamika na taarifa zao zipo mezani,na safari hii hakuna ujinga wa CCM kushindwa.Hapa Nyamagana kuna watu wanamvuruga mbunge ili kumuondoa, muda bado haujaisha.Wabunge na madiwani waheshimiwe ,waachwe wafanye kazi,”alisistiza Magoma.

Akizungumzia utaekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi alisema imetekelezwa ndani ya miaka mitatu na nusu ya uongozi wa Rais Magufuli kutokana na ualidifu na uzalendo wake wa kuhakikisha nchi inapata maendeleo ya kweli aliyoahidi wakati wa kampeni.

Alisema Rais Dk. Magufuli kwa aliyoyafanya ni dhahiri ameshaifanyia CCM kampeni kwa asilimia 80 hata kabla ya uchaguzi, hivyo ni jukumu la wana CCM kutafuta takwimu na kuwaeleza wananchi yaliyofanyika kwa sababu hakuna mwingine wa kuyasema lakini wakikaa kimya ni kutomtendea haki.

“JPM anastahili pongezi kwa namna alivyotekeleza ilani ya CCM katika muda mchache,amejenga miundombinu ya barabara km 12,885, fly over na Ubongo Interchange kwa bilioni 247,litajengwa daraja la Kigongo-Busisi (Milioni 700),amenunua ndege sita tayari,amelipa madeni ya watumishi sh. bilioni 595.2,”alisema Magoma.

Aliongeza kuwa amefanikiwa kujenga vituo vya afya 118, zahanati 522, hospitali 67 za wilaya ambapo 34 zimekamilika,ujenzi wa majengo ya ukaguzi wa elimu kote nchini kwa bilioni 15.2, umeme umeunganishwa kwenye vijiji 7,100, ujenzi wa mradi wa umeme Stiglers kwa Trilioni 6.5, Reli ya kisasa (SGR) kwa Trilioni 7 kwa fedha za ndani.

“Anataka Tanzania iwe nchi ya mfano ambapo bajeti ya mwaka huu ni Trilioni 33.11 kati ya hizo trilioni 12.15 za maendeleo, mikopo trilioni 2.52, bajeti ya dawa sh. milioni 415 (2019/2020) na elimu bilioni 450,”alisema Naibu Katibu Mkuu huyo wa Wazazi na kuhoji ,tulichelewa wapi kumpata Rais wa aina hii mwenye maono makubwa na nchi, uchumi unapanda.