Home Mchanganyiko BUNGE LA WANAFUNZI LAIBUA CHANGAMOTO KUHUSU BAJETI KUU YA SERIKALI

BUNGE LA WANAFUNZI LAIBUA CHANGAMOTO KUHUSU BAJETI KUU YA SERIKALI

0
 Mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya  Ntinko, Editha Mtinda akichangia hoja katika Bunge la   Wanafunzi wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Wilaya Singida Vijijini lililofanyika mjini Singida juzi.
Majadiliano yakiendelea.
************************
 
Na Dotto Mwaibale, Singida
 
BUNGE la Wanafunzi wa Shule za Msingi katika Halmashauri ya Wila ya Singida Vijijini limeibua changamoto zinazotakiwa kufikiwa na Serikali kupitia bajeti yake ya kila mwaka.
 
Changamoto hizo zilibainishwa mwishoni mwa wiki wakati wa majadiliano ndani ya bunge hilo liliketi kwa siku tatu mjini Singida ambalo  liliandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la Mtinko Education Development Organization (MEDO) kwa ufadhili wa Shirika la Norad kupitia ActionAid.
 
Akichangia hoja katika Bunge hilo lililowakilishwa na wanafunzi 40 kutoka katika halmashauri hiyo Editha Mtinda ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya  Ntinko alisema katika maeneo ya vijiji yenye watu wengi miradi mingi ya maendeleo imekuwa ikisuasua kutokana na bajeti inayotengwa kuwa ndogo na kutofika kwa kiasi kinachotakiwa.
 
“Bajeti inapotengwa kwenda katika maeneo hayo haifiki kama inavyotakiwa hivyo kusababisha miradi mingi ya maendeleo kama ujenzi wa shule, zahanati na miradi mingine kushindwa kukamilika” alisema Mtinda.
 
Mratibu wa Miradi wa Shirika hilo Iddy Mruma alisema walianzisha bunge hilo la wanafunzi ili waweze kuibua changamoto zilizopo katika maeneo wanayoishi na kuzionesha kwa serikali ili zifanyiwe kazi.
 
Alisema shirika hilo limekuwa likihimiza jamii kujenga tabia ya kulipa kodi itakayosaidia kuongeza ukubwa wa bajeti ya serikali pamoja na kuanzishwa kwa miradi inayopaswa kuhojiwa na kusimamiwa na jamii.
 
“Jamii inapaswa kuwa na uwezo wa kuhoji miradi yote inayofanywa na serikali katika maeneo yao  pamoja na kuisimamia” alisema Mruma.
 
Alisema bajeti inapotengwa inatakiwa kutoa kipaumbele kwa makundi kama ya wanawake na walemavu kutokana na makundi hayo kusahaulika mara kwa mara.