******************
MKUU wa Wilaya ya Ikungi, Mhe Edward Mpogolo amefanya ziara yake ya kwanza ndani ya Wilaya hiyo toka ateuliwa na Rais John Magufuli akichukua nafasi ya Miraji Mtaturu ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki.
DC Mpogolo amefanya ziara katika Kata nne za Iyumbu, Mgungira, Ighombwe na Mtunduru ambapo alitembelea miradi ya Maendeleo, kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi pamoja na kueleza mambo makubwa ambayo yamefanywa na Rais Magufuli tangu achaguliwe mwaka 2015.
Kero ambazo alikutana nazo na kuzitolea ufafanuzi ni changamoto ya maji, miundombinu ya barabara, uhaba wa vyumba vya madarasa, vituo vya afya, umeme na mawasiliano ambapo DC Mpogolo aliwaeleza wananchi hao hatua ambazo Serikali imezichukua katika kuzitatua.
” Ndugu zangu Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk Magufuli kwa kutambua mnakabiliwa na changamoto kwenye sekta ya afya tayari ameshatoa kiasi cha Shilingi Milioni 500 ambazo zitajenga kituo cha afya cha Iyumbu kitakachokua na uwezo wa kuhudumia kata zaidi ya tatu.
” Suala la Maji katika kata ya Mtunduru linaenda kuwa historia kwa maana ndani ya miezi miwili kutoka sasa kisima cha maji kitakamilika na kimegharimu zaidi ya Milioni 438, lakini kata ya Ighombe mkandarasi yupo site na ameshafikia kina cha maji kilichobaki ni kutengeneza Tanki LA kuhifadhia maji,” amesema DC Mpogolo.
Kuhusu elimu amewasifu wananchi wa kata zote nne alizotembelea kwa namna ambavyo wamekua wakijitoa kuchangia miradi ya maendeleo hasa katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ambapo amewaagiza wahandisi wa Wilaya kuhakikisha wanatoa ushauri katika miradi inayojengwa na wananchi ili kuifanya iwe bora zaidi.
Amewatoa hofu wananchi hao kuhusu changamoto ya umeme na kueleza kuwa Kata zote nne zipo katika mpango ww mradi wa umeme wa REA na kwamba ndani ya kipindi kifupi umeme utakua umewafikia.
” Ndugu zangu wana Ikungi suala la umeme katika kata hizi nne umekua ni changamoto. Nimelala hapa nimejionea. Niwahakikishie nimelichukua na kwa kushirikiana na wabunge wenu tutapambana kuuleta umeme ili kuongeza uzalishaji wa huduma za kijamii na kimaendeleo.
Nafahamu pia mna tatizo la mawasiliano, na mimi nimejionea kwa sababu nimefika hapa. Tayari Serikali ishatuma wataalamu wa minara na ninaamini hadi kufikia mwishoni mwa mwaka tutakua tumepata mawasiliano ambayo yataongeza ukuaji wa uchumi kwenye hizi kata zetu,” amesema DC Mpogolo.
Katika ziara hiyo DC Mpogolo aliambatana na watalaamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi ambapo pia aliweka kambi kwa kulala kwenye kila kata ambayo alifanya ziara lengo likiwa kujitambulisha na kusikiliza kero za wananchi wake.